Upinzani wakatalia mbali hazina ya miundombinu inayonuiwa ‘kufikisha Kenya Singapore’

UPINZANI umeomba Bunge kukataa Mswada wa Wizara ya Fedha kuhusu Miundombinu, 2026 na kusitisha mpango wa kuuza sehemu ya hisa za serikali katika Safaricom, ukisema mapendekezo hayo yanahatarisha ulinzi wa kikatiba wa fedha za umma na mali ya kimkakati ya taifa. Katika taarifa ya pamoja, viongozi wa upinzani waliitaka Bunge la Taifa la Kenya na Kamati yake ya Fedha na Mipango ya Kitaifa kutupilia mbali mswada huo mzima na Sera Nambari 3 ya 2025, inayopendekeza kupunguza umiliki wa serikali katika Safaricom. Upinzani pia umetaka uchunguzi huru wa kikatiba kuhusu pendekezo la hazina hiyo, pamoja na tathmini ya kina ya mali ya kimkakati kabla ya kupunguzwa kwa hisa za serikali katika kampuni hiyo ya mawasiliano, ambayo jukwaa lake la fedha kwa simu, M-Pesa, linaendesha sehemu kubwa ya malipo ya kidijitali na huduma za serikali. Kiongozi wa Wiper Democratic Movement, Kalonzo Musyoka, alisema hazina hiyo inayopendekezwa ni “suluhisho linaloleta tatizo,” akidai pengo la miundombinu nchini halitokani na ukosefu wa mifumo ya kifedha bali ni matokeo ya udhaifu katika utekelezaji wa miradi, ufisadi katika ununuzi na ukosefu wa uwazi wa kifedha. Alisema Kenya tayari ina zaidi ya hazina 60 ya umma nje ya Hazina Kuu nyingi zikiwa na majukumu yanayofanana na viwango vya chini vya uwajibikaji.