MVUTANO mkali umeibuka ndani ya chama cha ODM kufuatia uamuzi kwamba hakutakuwa na uchaguzi wenye ushindani wa maafisa wa kitaifa katika Mkutano Maalum wa Wajumbe wa Kitaifa (NDC) uliopangwa kufanyika Machi 27. Badala ya uchaguzi, ajenda ya mkutano huo imepunguzwa kuwa ya kuthibitisha maafisa wa muda walioteuliwa awali, hatua inayodaiwa kupangwa na mrengo unaomuunga kiongozi wa chama Oburu Oginga ili kuimarisha uongozi wake na kuzuia mgawanyiko zaidi ndani ya chama. Taarifa zinaonyesha kuwa chama hicho kinapanga kuitisha NDC nyingine Desemba mwaka huu au mapema 2027 kujadili ajenda nyingine muhimu, ikiwemo uwezekano wa kuidhinisha muungano wa kabla ya uchaguzi kati ya ODM na UDA ya Rais William Ruto. Uamuzi wa kupunguza ajenda ya mkutano huo ulipitishwa Jumatano na Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC), hatua inayofasiriwa kama mkakati wa kudhibiti mvutano unaoendelea kufuatia mabadiliko ya uongozi baada ya kifo cha aliyekuwa kiongozi na mwasisi wa ODM, Raila Odinga, Oktoba 2025. Hata hivyo, mrengo pinzani unaoongozwa na Katibu Mkuu Edwin Sifuna, Naibu Kiongozi Godfrey Osotsi, Gavana wa Siaya James Orengo na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino umetangaza kuwa hautashiriki mkutano huo iwapo nyadhifa zote za kitaifa hazitawaniwa kwa ushindani kidemokrasia. Seneta Osotsi alinukuu Katiba ya chama, hasa Ibara ya 47, inayoweka bayana mamlaka ya NDC ikiwemo kuchagua maafisa wa kitaifa, na kudai mzozo uliopo unaweza kutatuliwa tu kupitia uchaguzi wa wazi. Aidha, mrengo huo unataka orodha ya wajumbe wanaotarajiwa kuhudhuria ichapishwe mapema kwa ukaguzi wa umma, ikisema haiwezekani kuwa na NDC halali bila kukamilika kwa uchaguzi wa mashinani katika baadhi ya kaunti muhimu kama vile Nairobi na Kisumu. Kwa mujibu wa mpango wa sasa, maafisa wa muda waliothibitishwa na Baraza la Uongozi la Kitaifa (NGC) mjini Mombasa mwaka jana watawasilishwa mmoja mmoja mbele ya wajumbe kuthibitishwa au kukataliwa. Wanaotarajiwa kuwasilishwa ni pamoja na Dkt Oginga, manaibu wake watatu – Osotsi, Abdulswamad Nassir na Simba Arati pamoja na Mwenyekiti wa Kitaifa Gladys Wanga. Mwenyekiti wa ODM tawi la Nairobi George Aladwa amesema huu si wakati wa kufanya uchaguzi wa ushindani, akisisitiza kuwa uchaguzi wa mashinani lazima ukamilike kwanza kabla ya kufungua ushindani kuhusu nyadhifa za kitaifa. Alisema wanaotaka kuwania wanafaa wasubiri mkutano ujao kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027. Wakati huo huo, baada ya NEC kumvua Sifuna wadhifa wa Katibu Mkuu na kumteua naibu wake, Catherine Omanyo, kuushikilia, Jopo la Kutatua Mizozo ya Vyama lilitoa amri ya muda kuzuia utekelezaji wa uamuzi huo hadi kesi itakaposikilizwa na kuamuliwa. NDC ya ODM inaundwa na wanachama wa NEC, wabunge, magavana, wenyeviti wa matawi ya kaunti, pamoja na viongozi wa walio wachache na walio wengi katika mabunge ya kaunti. Katiba ya chama inaweka idadi ya wajumbe kuwa 3,000. Mkutano huo sasa unatazamwa kama kipimo muhimu cha mwelekeo wa ODM na mizani ya nguvu kati ya makundi hasimu, huku matokeo yake yakitarajiwa kuathiri mustakabali wa chama hicho kuelekea 2027.