MEYA ameshangaza wakazi kwa kutangaza mpango wa kujenga ukuta mkubwa kando ya barabara kuu ya N2 mjini Cape Town, hatua inayodaiwa kulenga kuzuia wahalifu wanaowalenga wasafiri na madereva wanaopita karibu na makazi duni ya jiji hilo. Meya huyo, Geordin Hill-Lewis, alisema ukuta huo ni sehemu ya mradi wa usalama unaojulikana kama N2 Edge Project. Mbali na ukuta huo, mpango huo pia utahusisha kuweka kamera za ulinzi, taa zaidi za barabarani, vizuizi vya usalama katika maeneo ya burudani na doria za ziada za polisi wa jiji. Hata hivyo, tangazo hilo limezua mjadala mkali miongoni mwa wakazi wa mitaa ya karibu kama Khayelitsha na makazi mengine ya mabanda yaliyo kando ya barabara hiyo. Wakazi wengi wanasema wamechanganyikiwa na uamuzi huo, wakidai mamlaka ya jiji inapaswa kwanza kutatua matatizo ya msingi yanayowakabili kila siku. Wanasema badala ya kutumia fedha nyingi kujenga ukuta, serikali ya jiji ingewekeza katika huduma muhimu kama makazi bora, maji safi, vyoo salama na miundombinu bora katika mitaa maskini ambayo kwa muda mrefu imekosa huduma za kutosha. Baadhi ya wakazi wanasema mpango huo unaonekana kama juhudi ya kulinda madereva na wasafiri wanaopita karibu na uwanja wa ndege badala ya kushughulikia changamoto za kijamii na kiuchumi zinazochangia uhalifu katika maeneo hayo. Hatua hiyo inajiri wakati serikali ya Afrika Kusini ikiendelea kukabiliwa na wimbi la uhalifu katika baadhi ya majiji. Hivi karibuni, Rais Cyril Ramaphosa aliwahi kupeleka wanajeshi katika jimbo la Western Cape kusaidia kudhibiti ghasia za magenge ya wahalifu. Licha ya changamoto hizo za usalama, wakazi wa maeneo maskini wanasema kujenga ukuta hakutamaliza tatizo la uhalifu. Badala yake, wanasisitiza kuwa suluhu la kudumu ni kuwekeza katika maendeleo ya jamii, ajira na huduma bora.