UPINZANI sasa unadai serikali imeteka sekta muhimu za kiuchumi, viongozi wakuu wakinyakua mali kiholela kiasi cha taifa kuendeshwa kama mali ya mtu binafsi. Aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ambaye pia ni kiongozi wa DCP, Makamu wa Rais wa zamani Kalonzo Musyoka na Mawaziri wa zamani Eugene Wamalwa na Justin Muturi wamewataka Wakenya wakomeshe mwenendo huo kwa kuuondoa utawala wa Kenya Kwanza katika uchaguzi mkuu ujao. Bw Gachagua alidai kuwa amepata habari kuwa wakandarasi kutoka China waliofaa kujenga reli jijini wamefurushwa ili makiritimba wa humu nchini watekeleze ujenzi huo ambao ufadhili wake ulitolewa na Uingereza. Alisema uamuzi huo uliafikiwa baada ya raia wa China kukata rufaa dhidi ya kunyimwa tenda hiyo. Kampuni hiyo China ilikuwa imenukuu gharama ya Sh22 bilioni huku mshindani wake aliyenukuu Sh29 bilioni akipewa zabuni hiyo. “Ninaomba serikali ya China ijiunge nasi kulalamikia hatua hii na naomba serikali ya Uingereza kuchunguza iwapo tofauti ya Sh7 bilioni itaenda mifukoni mwa watu walio serikalini,” akasema Bw Gachagua. Kiongozi huyo wa DCP alisikitika kuwa kwa sasa uchumi umebanwa ambapo sekta zinazofanya vizuri zinadhibitiwa na mtu mmoja. Alitaja saruji, vifaa vya kutengeneza sakafu, vyuma vya ujenzi, kama vifaa vya ujenzi ambavyo sasa uagizaji na mauzo yao yanadhibitiwa na mtu mmoja. “Sasa wameteka sekta za afya, madini, benki, jeshi, bima, elimu na sekta ya uchukuzi wa umma. Hii inaonyesha kwa nini sasa polisi wanatumiwa kutwaa mali ya watu ambao wanaonekana hawashabikii serikali kama Raphael Tuju.” “Huku Tuju akiondolewa kwenye mali yake kuna wamiliki wa vituo vya afya ambao pia wanahangaishwa ili wajiondoe kwenye biashara,” akasema Bw Gachagua. Alikuwa akiongea katika eneobunge la Gatanga katika ibada ya pamoja ya madhehebu mbalimbali eneo hilo. Mbunge huyo wa zamani wa Mathira alisema serikali inaweka juhudi zote kushinda uchaguzi mkuu wa 2027 ili kuuteka uchumi wa nchi kuwa mikononi mwa watu wachache watakaokuwa wakifanya maamuzi kuhusu urais katika kila kura. Bw Musyoka alisema hali ya sasa ya nchi ni ya kiwendawazimu, akisikitika kuwa umaskini unaendelea kuongezeka huku viongozi nao wakijilimbikizia mali. “Sasa serikali inarejesha kandarasi za Adani, kampuni ambayo ilikuwa ikilenga kuchukua uwanja wetu wa ndege,” akasema Bw Musyoka. Kiongozi huyo wa Wiper aliongeza kuwa kuna juhudi za kunyamazisha wakosoaji wa serikali na hilo linafanikishwa kupitia teuzi katika idara ya mahakama pamoja na Tume ya Uchaguzi (IEBC). “Ifahamike kuwa hatutakubali wizi wa kura kwa sababu tuna hiari ya kuendeleza maasi hata baada ya uchaguzi iwapo hatutaridhika na viwango vya uwazi uchaguzini,” akaongeza. Mbunge wa Nyali Mohamed Ali alisikitika kwamba sasa nchi inageuzwa kuwa mali ya mtu binafsi chini ya usimamizi wa mtu mmoja. Bw Wamalwa alilalama akisema kuwa nchi inahitaji Mungu ili kusimama na kupitia changamoto za sasa. “Utawala huu umevunja kila kitu. Kuanzia utekaji nyara na kuwaua wapinzani hadi wizi. Suluhu pekee ni kuondoa serikali hii kwa sababu nchi inaelekea pabaya sana,” akasema kiongozi huyo wa DAP-K. Bw Muturi alidai udhibiti wa sekta muhimu haujasaza Kaunti ya Murang’a akisema ardhi ya Delmonte ambayo ilifaa irejeshwe mikononi mwa umma imetwaliwa na wanyakuzi. Alisema alipokuwa Spika wa Bunge la Kitaifa, wabunge waliidhinisha ardhi hiyo ipewe maskwota 4,000 lakini hilo halijafanyika. “Tukichukua mamlaka, tutahakikisha kwamba wakazi wa Murang’a wanapata haki kwa kupewa ardhi yao,” akasema Bw Muturi. Wiki jana, Bw Muturi alidai kuwa watu wanaohusishwa na serikali walikuwa wakijaribu kuchukua umiliki wa hospitali ya Nairobi Hospital. Wikendi Mwenyekiti wa Bodi ya hospitali hiyo, Dkt Job Obwaka, naibu wake Wakili Samson Kinyanjui na mwenyekiti wa zamani Dkt Chris Bichage walikamatwa na kuzuiliwa kwa tuhuma za kughushi usajili wa wanachama wa taasisi hiyo.