TUNAPOTUNGA sentensi sharti tuzingatie uandishi sahihi wa maneno. Iwapo mwandishi atafanya kosa la kutoandika maneno sahihi katika sentensi, ujumbe aliokusudia kuwasilisha kwa hadhira yake unaweza kukosa kueleweka kama alivyotarajia. Baadhi ya wanafunzi wana mazoea ya kuunganisha maneno mawili yasiyofaa kuunganishwa kuwa neno moja. Iwapo maneno yakiunganishwa hayataunda nominoambata ambazo huundwa kwa kuunganisha maneno mawili, ni kosa kuunganisha maneno hayo. Changamoto ya kuunganisha maneno mawili kuwa neno moja hasa hujitokeza palipo na neno la herufi chache kama vile herufi mbili au tatu. Mfano ni palipo na kiunganishi na na kwa. Mara kwa mara utapata sentensi kama vile: *Tulifaulu katika masomo kwasababu tulitia bidii. *Kwanini umechelewa kufika shuleni? *Wakenya wanajukumu la kuyatunza mazingira. Sentensi hizi iwapo zinaeleweka zina makosa ya kuunganisha baadhi ya maneno kuwa maneno mawili. Tunafaa kusema: Tulifaulu katika masomo kwa sababu tulitia bidii. Kwa nini ulichelewa kufika shuleni? Wakenya wana jukumu la kuyatunza mazingira. Maneno mengine ambayo baadhi ya wanafunzi hutatizika wanapoyaandika ni: Kwakweli badala ya kwa kweli, wakwanza badala ya wa kwanza, halikadhalika badala ya hali kadhalika, kwahivyo badala ya kwa hivyo na kwakuwa badala ya kwa kuwa. Mwanafunzi mwenye changamoto ya kuunganisha maneno mawili kuwa neno moja anafaa kufanya mazoezi ya kutamka maneno hayo, kuyaandika mara kwa mara kisha kuyatumia maneno hayo kutunga sentensi sahihi.