MGHAMBONYI, TAITA MKE wa lofa mmoja kijijini hapa, alilazimika kuitisha kikao cha dharura cha wazee ili kumrai mumewe aache kulala mvunguni mwa kitanda. Kulingana na mke huyo, mumewe amekuwa akilala mvunguni na kumuacha kuvumilia kibaridi kikali usiku kucha kitandani. Kila alipouliza mumewe hata haki yake ya chumbani, jombi alidai yuko kwenye maombi maalum ambayo miongoni mwa matakwa ni yeye kulala mvunguni mwa kitanda na kutoshiriki tendo la ndoa na mkewe. Ilifikia mahali mke alichoshwa na mienendo hiyo. Siku ya kikao ilipofika, wazee walikusanyika bomani na kumuuliza jombi huyo maswali mbele ya mkewe naye akafunguka. “Nilipogundua huyu mke wangu niliyempenda na kumthamini analala na mubaba kijijini niliamua kulala mvunguni ilmradi nisusie hilo tunda lake. Wacha mubaba aendelee kulimega na kulichafua. Sitalimenya tena ila sitamwacha hadi kifo kitakapotutenganisha,” Lofa akasema.