Anachuma hela kama njugu kwa kuchakata divai ya hibiscus

TEDDY Fidelis Lyimo anainua glasi polepole, anamimina divai ya rangi ya waridi iliyochanganyika na nyekundu kisha anakunywa funda kiasi huku akitabasamu inapoteremka kooni. Kinywaji hicho kinaonekana kung’aa na kufurahisha anapokishabikia. “Hii ina umri wa mwaka mmoja. Ina uchachu mdogo unaoifanya iwe safi na yenye ladha nzuri,” anaeleza. Baadaye anachukua chupa nyingine—ya zamani na yenye thamani zaidi. Anapomimina, rangi inaonekana kuwa tofauti. “Divai hii si nyekundu tena bali imegeuka rangi na kuwa ya dhahabu yenye mchanganyiko wa waridi, ishara ya kukomaa zaidi. Hii ina umri wa miaka mitatu,” Fidelis anafafanua. Kulingana na mjasiriamali huyu, kadri muda unavyopita, divai hukomaa zaidi kiladha na thamani. Ikiachwa kuchacha kwa muda mrefu, ndivyo bei yake inavyoongezeka. Hata rangi yake inaweza kuanza kufanana na whisky. Hii ndiyo kazi ya kila siku ya Fidelis, mmiliki wa kampuni ya North East Wine Tanzania iliyoko Jijini Arusha. Aidha, biashara yake inaunda divai kwa kutumia maua ya hibiscus—zao ambalo anaamini limepuuzwa kwa muda mrefu ukanda wa Afrika Mashariki. “Hibiscus haijapuuzwa Tanzania au Kenya tu, bali katika eneo lote la Afrika Mashariki. Ni zao lililosahaulika,” anasema. Tofauti kuu kati ya divai ya hibiscus na divai ya zabibu iko kwenye malighafi. [caption id="attachment_185935" align="aligncenter" width="300"] Teddy Fidelis Lyimo, mmiliki wa kampuni ya North East Wine Tanzania iliyoko Jijini Arusha akionyesha divai ya hibiscus anayounda wakati wa East African Youth in Agri-Food Systems Expo 2025 (EAYASE-25), maonyesho ya kilimo na kibiashara yaliyofanyika Nairobi kuanzia Desemba 3 hadi 5, 2025. Picha|Sammy Waweru [/caption] Divai ya hibiscus hutengenezwa kwa kutumia maua ya hibiscus, huku divai ya kawaida inayojulikana na wengi hutokana na zabibu, ambazo ni matunda. Tofauti hii huathiri ladha, harufu na hata thamani na virutubisho. Afrika Mashariki, hibiscus hulimwa kwa minajili ya chai, juisi na mapambo. Kenya, Tanzania na Uganda ni miongoni mwa wazalishaji wakuu wa zao hili kutokana na hali nzuri ya hewa, udongo na ongezeko la mahitaji ya vinywaji vyenye afya. Hata hivyo, kwa miaka mingi zao hili limekuwa likitumika kwa kiwango cha chini nchini Tanzania. Kulingana na George Mathenge, mtaalamu wa masuala ya sayansi ya chakula na lishe katika Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), hibiscus ina thamani kubwa kisiha. “Ni zao lenye virutubisho vingi na husaidia kudhibiti shinikizo la damu (blood pressure). Wagonjwa wengi hushauriwa kunywa sharubati, chai ya hibiscus au hata kwa kuitia kwenye maji moto,” anasema mtaalamu Mathenge. Fidelis aliamua kubadilisha mtazamo huo mwaka 2020, wakati janga la Covid-19 lilipotua Kenya, Tanzania, Uganda, bara la Afrika na ulimwengu kwa jumla na kutatiza na kufunga biashara nyingi, hatimaye likamfanya apoteze kazi. “Kilikuwa kipindi kigumu sana. Nilikuwa na akiba kidogo niliyokuwa nimeweka. Badala ya kusubiri kupata kazi nyingine na kuambulia patupu, niliamua kuwekeza kwenye uchakataji wa hibiscus,” anaelezea. Kwa mtaji wa Sh2 milioni, thamani ya Tanzania, alinunua malighafi na vifaa vya msingi kumuwezesha kuanza safari. [caption id="attachment_185936" align="aligncenter" width="300"] Kando na divai, Teddy Fidelis Lyimo ameanza kuchakata whisky ya hibiscus inayojulikana kama East Maruwa. Picha|Sammy Waweru [/caption] Mwanzoni, kwenye mahojiano na Akilimali alidokeza kwamba alifanya kila kitu mwenyewe: kutafuta hibiscus, kuisafisha, kuifanya ichache – kuchakata, kupakia kwenye chupa na kutafuta wateja yaani soko. Jaribio lake la kwanza alikadiria hasara kubwa ambapo anafichua kupoteza lita 1,000 za divai kutokana na hitilafu katika uchachushaji. “Hata hivyo sikukata tamaa. Nilifanya utafiti wa kina na kurekebisha makosa niliyofanya,” Fidelis akasema. Leo hii kampuni yake huzalisha zaidi ya lita 2,000 za divai ya hibiscus kila baada ya miezi mitatu na imeajiri watu watano. Wateja wake sasa wanatoka Tanzania, Kenya, Sudan Kusini na Uganda. Kando na divai, ameanza kuchakata whisky ya hibiscus inayojulikana kama East Maruwa. Maonyesho ya kibiashara Tanzania, Kenya, Uganda na Tanzania yamekuwa jukwaa lake kuhamasisha soko la divai yake. Aidha, Fidelis alikuwa miongoni mwa walioshiriki East African Youth in Agri-Food Systems Expo 2025 (EAYASE-25), maonyesho ya kilimo na kibiashara yaliyofanyika Nairobi kuanzia Desemba 3 hadi 5.