MAGAVANA watatu wanaohudumu muhula wa kwanza Luo Nyanza, wanakodolewa macho na upinzani mkali kuelekea uchaguzi wa 2027 ambao utakuwa wa kwanza bila marehemu Raila Odinga. Magavana Ochilo Ayacko (Migori), James Orengo (Siaya) na Gladys Wanga (Homa Bay) wanatokwa jasho kwenye azma ya kusalia afisini 2027 kutokana na kuchipuka kwa maasi makubwa dhidi ya utawala wao. Ni Gavana wa Kisumu Profesa Anyang’ Nyong'o ambaye anahudumu muhula wake wa pili na kikatiba haruhusiwi kugombea tena ugavana mwaka ujao. Kwa miaka mingi, mkondo wa siasa za Nyanza ulikuwa ukiamuliwa na marehemu Raila Odinga kupitia chama cha ODM. Hata hivyo, mauti ya Bw Odinga, yamewaacha viongozi wengi waliokuwa wakiningínia kwenye koti lake na kutegemea umaarufu wake kushinda viti, mayatima. Kaunti za Luo Nyanza zilikuwa zikishuhudia ushindani mkali kuelekea mchujo wa ODM na mara nyingi ilikuwa ikimlazimu Raila kuingilia kati kuzima moto wa uhasama na kukumbatia siasa za maelewano. Kuelekea uchaguzi mkuu uliopita, Kaunti ya Homa Bay ilishuhudia ushindani mkali wa tikiti ya ODM kati ya aliyekuwa Naibu Gavana Oyugi Magwanga na Bi Wanga. Uhasama kati ya wawili hao ulifikia kilele mwezi uliopita baada ya Bw Magwanga kujiuzulu akisema hawezi kuvumilia hujuma alizodai zilikuwa zikitoka kwa bosi wake. “Tofauti zetu haziwezi kutatuliwa kwa sababu zinatokana na masuala ya uongozi, uwajibikaji na ahadi ambazo tulitoa kwa raia wakati wa kampeni,” akasema Bw Magwanga baada ya kujiuzulu Februari 27. Mbunge huyo wa zamani wa Kasipul sasa anaendeleza kampeni kali mashinani akiwataka wakazi wa Homa Bay wamchague mnamo 2027. Bw Ayacko hapumui kutokana na ubabe mkali wa kisiasa wa Mbunge wa Uriri Mark Nyamita na mwenzake wa Suna Magharibi. Wafuasi wa Bw Ayacko na Nyamita hukabiliana sana katika hafla za mazishi na umma, na mara si moja makabilianom hayo yameishia majeraha. Bw Nyamita amekuwa akizunguka sehemu mbalimbali za Migori akisema Bw Ayacko anastahili kuhudumu muhula moja pekee kutokana na utendakazi duni. Mnamo Februari 14, watu sita walisalia na majeraha ya risasi mwilini baada ya Gavana Ayacko na Bw Masara kujibizana vikali. “Nitamtafuta Ochilo hadi kwenye chumba chake cha kulala na lazima nimtie adabu. Ajitokeze na akabiliane na mimi na kama ni fujo ndiyo itasababisha atoke ugavana, niko tayari,” akasema Bw Masara huku akimwonya gavana huyo dhidi ya kukanyaga eneobunge lake. Bw Orengo naye hana lake kwa kuwa anaegemea mrengo wa Linda Mwananchi ambao unapinga uongozi wa Dkt Oburu Oginga katika ODM. Tayari uongozi wa ODM unaonekana kukumbatia mbunge wa zamani wa Rarieda Nicholas Gumbo kuwania wadhifa huo. Bw Gumbo ambaye alishindwa na Bw Orengo 2022, amerejea ODM na amekuwa akishiriki mikutano ya Linda Ground. Pia ODM imeanzisha ushirikiano na Naibu Gavana wa Siaya Oduol Denge ambaye haonani na Bw Orengo na hata kwa kipindi kimoja aliondolewa madarakani na madiwani kabla ya kuokolewa na Seneti.