SHAIRI: Lala pema Khamenei

Kwa jina lake Karima, Yarrabi Allah Manani, Natetema natetema, aloyafanza shetwani, Wa Marekani mnyama, na nguruwe mzayuni, Walovamia Irani, wakamuua mwandani. Unyama huo unyama, ukafiri ufatani, Walofanza zao njama, vigaro vya tini tini, Kwa Mola wana lawama, wataingia motoni, Khamenei wa Irani, tutakuenzi daima. Nafasi uliwanyima, kupora vilivyo ndani, Mafuta yenu heshima, walotaka hayawani, Si wa mbele ni wa nyuma, wauaji namba wani, Khamenei wa Irani, tutakuenzi daima. Wachukia Isilama, si leo tangu zwamani, Gaza huko wakachoma, mali vitu vya thamani, Na bado hawajakoma, siku ni arobaini, Khamenei wa Irani, tutakuenzi daima. Yalo mangi sitasema, Joka narudi Pangoni, Na chombo hakitazama, chaelea baharini, Iko siku watakwama, ishanena Quruwani, Khamenei wa Irani, tutakuenzi daima. THABIT POPPATS HASSAN AL USTADH JOKA KUU KWALE Upendo wa kweli Ukiipata bahati, ya kupendwa na mwenzio, Jaribu kujidhibiti, usimpeleke mbio, Sababu penzi la dhati, ni chamcha na chajio, Upendo wa kwelikweli, huwa watoka moyoni. Kutikisa kibiriti, ni kuanza usanii, Umkalie chapati, mwenzi awe hasikii, Umpe pendo la dhati, kisha uwe hutulii, Upendo wa kwelikweli, huwa watoka moyoni. Upendo wa kweli sera, ndio hujenga imani, Kupenda mtu kwa sura, kwaondosha tumaini, Hata vazi la kung'ara, halina upendo ndani, Upendo wa kwelikweli, huwa watoka moyoni. Hata kama ni mrembo, mzuri unashaini, Tabia ikiwa kombo, binti hauna thamani, Upendo ndio ulimbo, kwengine mtu haoni, Upendo wa kwelikweli, huwa watoka moyoni. Kisha na yako tabia, iwe nzuri ya shani, Usiwe mwenye udhia, mumeo kumrubuni, Binti hebu nisikia, nisemayo Luqmani, Upendo wa kwelikweli, huwa watoka moyoni. Huwa watoka moyoni, upendo wa kwelikweli, Hautoki ubavuni, kwenye pafu na akili, Hakika wenye thamani, lasema shairi hili, Upendo wa kwelikweli, huwa watoka moyoni. Hizi zote dalidali, huwa ni za ujanani, Kufungiana kufuli, eti mko mapenzini, Kumbe wote ni uchali, mapenzi yako moyoni, Upendo wa kwelikweli, huwa watoka moyoni. LUDOVICK MBOGHOLI AL - USTADH - LUQMAN NGARIBA MLUMBI Nawatakia fanaka Wanafunzi wangu wote, ninawaombea heri, Wasipatwe na lolote, wabaki kuwa wazuri, Wanaoishi kokote, Mungu awape sitiri, Watoto wa St. Jude, nawatakia fanaka. Na kwa gredi ya sita, nataka watu wasome, Na nyote ninawaita, ili uzembe ukome, Ni kiboko nitaleta, nitawachapa mkeme, Nawatakia fanaka, watoto wa St. Jude. Na wa gredi ya saba, ya nane hadi ya tisa, Na nyinyi ombeni toba, na mjibidishe sasa, Na majibu kuyaiba, hii muache kabisa, Nawatakia fanaka, watoto wa St. Jude. Na hapa natuma salamu , mamaa wetu mwandani, Na hata pia walimu, wote walio shuleni, Nataka kuwasalimu, na pongezi abadani Nawatakia fanaka, watoto wa St. Jude. STEPHEN DIK ODANGA MWALIMU MPENDA USHAIRI, ST JUDE EDUCATIONAL CENTRE, VOI Buriani Mbunge Ng'eno Lo! Janga kuu natowa, kwayo fani umalenga, Hayawi hayawi huwa, kuntu kaamba wahenga, Taifa nzima makiwa, megubikwa nalo janga! Ewe marehemu Ng'eno, Mola amlaze pema. Ajali ndege ndo kawa, yayo maafa nalonga, Eneo Nandi twelewa, woi! Kazuka visanga! Lo! Kifo kamchukuwa, haki Kenya alojenga, Ewe marehemu Ng'eno, Mola amlaze pema. Shujaa kanyemelewa, na mauti soyapinga! Ndo ndege loabiriwa, jama! Safari kafumba, Bungeni mtegemewa, kenda njia asopanga! Ewe marehemu Ng'eno, Mola amlaze pema. Mauti mbi kaambiwa, safariye kaboronga! Laiti sisi tungekuwa, kifoche tungekitinga! Kinara aloenziwa, na wazee kwa wachanga, Ewe marehemu Ng'eno, Mola amlaze pema. Mtetezi wetu kawa, bingwa kono tulounga, Shujaa asotugawa, kyongozi loleta mwanga, Mwanaharakati juwa, kifo kwi'shi memtenga! Ewe marehemu Ng'eno, Mola amlaze pema. La kihoro tukapewa, kutangaziwa matanga! Do! Kifo kuntu kajiwa, maisha yake katinga! Mauti mawi yakawa, bingwa kupiga chenga! Ewe marehemu Ng'eno, Mola amlaze pema. Habari kaandaliwa, ya rungoya na runinga, Magazeti ka'ndikiwa, kaghani nao malenga, Adha lipotangaziwa, majonzi katanda anga! Ewe marehemu Ng'eno, Mola amlaze pema. Kenya nzima megumiwa, kilio mato metunga, Majonzi inna kajawa, twahisi kama kimbunga, Twamini tumetendewa, kwibiwa haki lokinga, Ewe marehemu Ng'eno, Mola amlaze pema. Wapi kifo kakosewa, kumwiba ja kifaranga? Kwishi kyongozi sifiwa, kifoche katia nanga! Wakenya kahudumiwa, kisheria tukasonga, Ewe marehemu Ng'eno, Mola amllaze pema. Menena yaso afuwa, ni vyema pate kufunga, Sote kuntu megumiwa, u mwiba ulotudunga! Rabi weze kumwokowa, juhudi mzo lolenga, Ewe marehemu Ng'eno, Mola amlaze pema. JAMES MUTWIRI WANJAGI, "MALENGA MSIFIKA NA MSIKIVU," CHUKA, THARAKA- NITHI Mvua ni baraka Yamesikika maombi, haraka yakajibiwa, Litutesa sana vumbi, mashaka ikatujawa, Jua likakita kambi, siku masiku ikawa, Mvua kwetu baraka, Maulana amejibu. Tulikosa hata maji, leo hii tumepata, Mijini hata vijiji, taabu zilitupata, Leo tunayo meseji, kwote Kenya kumetata, Mvua kwetu baraka, Maulana amejibu. Wakulima amukeni, wakati umewadia, Upanzi kazi shambani, mbegu zinawalilia, Zimechoka paketini, kila siku kutulia, Mvua kwetu baraka, Maulana amejibu. Mifugo zinafurahia, chakula mepatikana, Imani mewafikia, wamepata yao mana, Tuhifadhi zosalia, kesho pia namaana, Mvua kwetu baraka, maulana amejibu. Mazingira inacheka, tabasamu yafuraha, Mimea itachipuka, tanawiri si mzaha, Yafanisi ikifika, wino nimemaliza Shaha, Mvua kwetu baraka, Maulana amejibu. WACHIRA ROMEO MUGO MALENGA LANGU JICHO CHUO KIKUU CHA MURANG'A Aina za maneno Nomino hutaja jina, hishima yake ipeni, mifano ya kuwiana, imejaa duniani, madhali tunafunzana, weka hii akilini, kitu, mtu na mahali, kitenzi hata na hali. Kivumishi hueleza, kuhusu hii nomino, aghalibu hutujuza, sifa za kubaliano, milikaji kijasaza, vashiria kwa mikono, shairi hili ni sawa, hili hapa ni mfano. Kitenzi ndiyo shughuli, mwili huushirikisha, matukio chakubali, kisha kuyakaribisha, kina zake sampuli, kidogo nakuonjesha, kikuu, kisaidizi, pamwe na kishirikishi. Kihusushi wakijua? uhusiano hujenga, usiwahi ingilia, la sivyo kitakutenga, kaziyo twafurahia, kongole kwa kutuunga, juu ya, kwenye katika, hadi, tangu na vingine. Kunganishi acha wivu, sitoweza kukuata, ninakiri huna uovu, uyafanyayo ni beta, uzidi ukiongoza, mara tisini na sita, walakini, bila shaka, ingawa na kadhalika. Visifa ni vielezi, si unavofikiria, hii ndiyo yake kazi, akika hufafanua, matukio kwa ujuzi, sarufi kizingatia, hujibu maswali haya, marangapi, vipi, lini... Viwakilishi kongole, wakilisha pasi hofu, mifano nawaletile, niloipanga sufufu, yaloandikwa ni tele, vitasomwa maradufu, mleo na kiishiyo, njuga ukaivaliye. ELISHA OTOYI [ISAH BIN OMAR] “MALENGA WA WANYONGE” HOMABAY