HATIMAYE chama cha Pamoja African Alliance kimeamua kujiunga na kile cha Rais William Ruto cha UDA na kutangaza rasmi kwamba hakitasimamisha mgombea yeyote kwenye uchaguzi mkuu wa 2027. Spika wa Bunge la Seneti Bw Amason Kingi, alitangaza kuwa chama hicho hakitasimamisha mgombea yeyote wa kisiasa kwenye uchaguzi ujao. Bw Kingi ambaye alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa chama hicho, alisema uamuzi huo uliafikiwa kufuatia mazungumzo kati yake na Rais William Ruto wa chama cha UDA. “Mwaka wa 2022 tulipitapita sana hapa tukiuza chama cha PAA na tulikuwa na wagombea katika viti mbali mbali. Hata mgombea wetu wa ugavana wetu wa Kilifi alikuwa wakili George Kithi. Najua wengine wataniuliza ni vipi tena lakini leo ninasimama mbele yenu kuwaeleza kuhusu 2027,” alisema Bw Kingi. Bw Kingi alielezea wakazi wa Kilifi kwamba walishauriana na Rais kwamba wataelekea uchaguzi mkuu wakiwa kitu kimoja. Alisema alihusisha viongozi wa nyanjani kuhusu mikutano hiyo na kuafikia kuzama kwenye UDA. Haya yanajiri siku mbili tu baada ya Rais Ruto kukutana na viongozi wa Pwani katika hafla ya Iftar katika Ikulu ya Mombasa. Kwenye mkutano huo, Bw Kingi alimhakikishia Rais Kwamba atashirikiana na Waziri wa Michezo na Vijana Bw Salim Mvurya kumtafutia kura milioni 3 zilizoko eneo la Pwani. "Nitazunguka kaunti zote za Pwani kuhamasisha Wapwani kuchukua kadi za kura ilitukupatie kura zote. Utarithi kura ambazo Wapwani wamekuwa wakimpigia aliyekuwa kinara wa ODM, marehemu Raila Odinga," alisema Bw Kingi. Alisema chama cha UDA kimepata umaarufu mkubwa katika Kaunti ya Kilifi huku akimpigia debe aliyekuwa Waziri wa Jinsia Bi Aisha Jumwa. Bi Jumwa alishatangaza kuwa anawania ugavana wa Kaunti ya Kilifi kupitia chama cha UDA. Atamenyana na Gavana Gideon Mung’aro wa ODM. “Tunataka chama cha UDA kiendelee kupata umaarufu zaidi. Tunataka chama cha UDA kipate viti vingi vya kisiasa, tuna mwaka mmoja tu kuhakikisha tunapata nguvu nyanjani. Tuanze kuimba wimbo wa UDA kila mahali. Tunataka Mbunge wa Magarini na Gavana atoke kwenye chama cha UDA,” alisema Bw Kingi. Aliwaonya wanasiasa dhidi ya kuhamahama kwenye vyama akiwataka wasalie katika chama cha UDA. Spika Kingi alisema atahakikisha anafunga Pwani ili mrengo wa upinzani unaoongozwa na Bw Rigathi Gachagua usipate nafasi ya kunyemelea kura za eneo hilo. Hata hivyo, Rais aliwataka viongozi wa Pwani kushirikiana na kuacha migogoro na ubabe wa kisiasa. Hii ni baada ya Waziri Hassan Joho wa Madini na Uchumi wa Baharini na mwenzake Bw Mvurya kuanza kugombana kuhusu kiti cha unaibu wa Rais. Bw Joho amekuwa akimezea mate kiti hicho huku Bw Mvurya akimuonya dhidi ya tamaa hiyo akimwambia Rais ndiye mwenye uwezo wa kuchagua mgombea mwenza.