Ruto, Upinzani waweka ustaarabu kando na kunyesheana makombora ya kudhalilisha

RAIS William Ruto jana alitumia ziara yake Magharibi mwa Kenya kushambulia vikali viongozi wa upinzani na kufungua malumbano makali ya kisiasa. Kilichoanza kama ziara ya maendeleo kilibadilika haraka baada ya rais kuvua nembo ya kiongozi wa kitaifa anayetarajiwa kuzungumzia sera na maendeleo na kuanza mashambulizi ya kisiasa dhidi ya wapinzani wake. Jukwaa ambalo mara nyingi hutumika kuzungumzia sera na maendeleo liligeuka kuwa uwanja wa maneno makali ya kisiasa, huku lugha ya uongozi ikipisha ile ya matusi. Katika kituo chake cha kwanza Cheptais, eneo la Mt Elgon katika Kaunti ya Bungoma, rais alionekana kuweka wazi kuwa hatavumilia tena mashambulizi ya kisiasa bila kujibu. “Ati wale majamaa wa upinzani, ajenda yao ni moja tu, William Ruto. Kama mnataka tuende hapo mimi niko tayari. Lakini kwa sababu niko na shughuli za maendeleo, nitawapa asilimia moja ya muda wangu, asilimia 99 ni kwa watu wa Kenya,” alisema Rais Ruto. Katika hotuba zake za siku nzima, rais aliwashambulia wapinzani wake kwa maneno makali akiwaita wapumbavu, matapeli, walaghai na watu wasiostahili kushindana naye katika uchaguzi mkuu ujao. Mashambulizi yake ya kwanza yalionekana kumlenga naibu kiongozi wa chama cha Jubilee na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i, ambaye alimkejeli na kumtaka aende mazoezini kabla ya kumkabili kisiasa. “Jana, walisema mimi ni mwembamba na sipati usingizi wa kutosha. Mimi najua wakati wa kupunguza uzito ili nijikite kwenye kazi yangu. Angalieni vioo mjione, muende kwa mazoezi kwanza kwa sababu matumbo yenu yanakaribia kupasuka,” alisema Rais Ruto. Baada ya kauli hiyo, picha zinazomuonyesha Dkt Matiang’i akilala katika mikutano ya hadhara zilianza kusambaa mitandaoni. Rais pia alimkosoa kiongozi wa chama cha Democratic Action Party of Kenya Eugene Wamalwa akisema alirithi tu nafasi ya kisiasa ya marehemu kaka yake Michael Kijana Wamalwa na anapaswa kujijenga kisiasa. “Iko mwingine hapa Kitale, hata sijui aliachiwa kiti na ndugu yake. Utaongoza nchi aje na huwezi kuongoza boma lako? Enda jenga nyumba kwanza na utafute bibi uachane na mimi,” alisema rais. Aidha, Rais Ruto alimshambulia aliyekuwa naibu wake na sasa kiongozi wa chama cha DCP Rigathi Gachagua akimlaumu kwa madai mbalimbali ya uhalifu na migogoro ya familia. Bw Gachagua naye alimtaka Rais aache kulipuka kwa hasira kwa kuwa wanafichua ufisadi katika serikali yake. “Tabia ya uporaji na wizi wa kiwango cha Mobutu Sese Seko inayoshuhudiwa nchini Kenya lazima ikome, bila kujali hasira au vitisho vinavyojitokeza! Lazima ikome! Tutawaumbua na kuwafichua wote wanaohusika bila ubaguzi. Tutakabiliana na mbinu za udikteta wa ujanja na wa kizamani bila kujali kelele au vitisho vitakavyotolewa,” aliandika katika X. Katika majibu yake jana, Dkt Matiang’i alisema alishtushwa na matamshi ya Rais Ruto dhidi ya viongozi wa upinzani, akijiuliza kwa nini rais anajali sana kuhusu wanachokula. “Rais wetu mimi namheshimu, na naheshimu ofisi yake. Ndiyo maana mimi sijaongea mambo yake mbeleni. Lakini leo ameanza sasa kututusi sisi, watu wote wa upinzani,” alisema. Aliendelea kusisitiza kuwa Kenya, inastahili uongozi unaozingatia masuala muhimu ya kitaifa badala ya mashambulizi ya kibinafsi kuhusu chakula au umbo la mwili. “Yaani nchi yetu leo, zaidi ya miaka 60 baada ya uhuru, katika kiwango cha kampeni za urais tunaanza kuzungumzia mambo ya nani anakula nini. Ati nani anakula zaidi, nani anakula wapi. Ninasema haya kwa uchungu mwingi,” alisema. Bw Matiang’i pia alitetea tabia zake za ulaji kwa mzaha, akitaja safari zake Kisii kula vyakula vya kienyeji, huku akihoji kwa nini rais anaonekana kusumbuliwa na kile anachokula.