VISA kadhaa vimeibuka kuhusu watu kuwekewa dawa kwenye vinywaji na kupoteza pesa katika Mashindano ya Safari Rally (WRC) yaliyofanyika Naivasha wikendi. Mashindano hayo ya siku tatu yanayofanyika kila mwaka ambayo ni sehemu ya tamasha mashuhuri ya 2026, yalivutia maelfu ya mashabiki kutoka kote nchini na kwingineko. Huku msisimko na sherehe zikipamba moto, watu kadhaa baadaye waliripoti kuwekewa dawa na wahusika wasiojulikana kabla ya kupoteza kiasi kikubwa cha pesa, simu na mali nyingine ya kibinafsi. Mhasiriwa mmoja aliyesimulia masaibu yake akichelea kutajwa, alisema alipoteza Sh80,000 pesa taslimu alizokuwa amebeba kujiburudisha katika hafla hiyo wikendi. Alisema kabla ya kupoteza fahamu, aliingia kituo maarufu cha burudani na marafiki wake wawili aliosafiri nao Naivasha kufurahia WRC. “Kando yetu kulikuwa mabinti wawili waliojishughulisha na mazungumzo ya kina na yamkini hawakuwa na haja ya tulichokuwa tunafanya. Hatukujua walikuwa wanatuhadaa ili tusijue nia yao,” alisimulia. Mhasiriwa alisema anakumbuka tu akiamka saa kadhaa baadaye akiwa amechanganyikia alipogundua kila kitu cha thamani alichokuwa nacho kimetoweka. “Ninachojua ni kwamba niliamka siku iliyofuata nikiumwa na kichwa na bila chochote mifukoni mwangu. Nilienda hapo kufurahia mashindano ya magari, lakini niliondoka bila kitu,” alisema. “Simu yangu, kibeti cha pesa na pesa zote zilitoweka. Ni lazima walituwekea dawa tulipoenda uwanja wa densi.” Mwanamke aliyehudhuria moja kati ya vituo vya burudani karibu na sehemu za mashindano hayo Jumamosi, alisema alianza kuhisi kisunzi baada ya kukubali kinywaji kutoka kwa mtu waliyekutana naye. Alisema tukio hilo lilimgutusha na kumlazimu kukatiza ziara yake fupi Naivasha, na kurejea nyumbani kuuguza masaibu yake ya kupoteza mali ya thamani na hela. “Nilihisi ghafla usingizi na kuwa mnyonge. Nilipoamka saa kadhaa badaaye, mkoba wangu ulikuwa umetolewa kila kitu ikiwemo simu yangu. Ilibidi niombe simu na kuwapigia marafiki zangu waliokuja kunichukua. Si hayo nilikuwa nimeendea Naivasha,” alisema. Taifa Leo ilipozungumza nao Jumatatu hawakuwa wameripoti visa hivyo kwa polisi wakisema watadhihakiwa. Kamanda wa Polisi Naivasha Wilson Sigei alisema hakuna ripoti rasmi zimewasilishwa kwa polisi kuhusu malalamishi yanaohusiana na kutiliwa dawa katika WRC wikendi. Bw Sigei alitoa wito kwa wanaoamini huenda walikuwa wahasiriwa wa uhalifu huo kupiga ripoti katika kituo cha polisi kilicho karibu ili uchunguzi uanze.