Mbinu nafuu ya kiasili inayosaidia katika utunzaji wa vifaranga

ENEO la Tuigoin katika Kaunti ya Trans-Nzoia, linafahamika kwa hali nzuri ya hewa inayochangia ukuzaji wa aina mbalimbali ya vyakula na ufugaji wa wanyama. Pauline Sambu, ni mmoja wa wakazi wa eneo hilo. Yeye huuza vifaranga. Tunapomtembelea, anafunguka jinsi aina hii ya biashara inamfaidi sio yeye tu, bali pia vijana na akina mama ambao wameamua kujikita kwenye ufugaji wa kuku ili kujiendeleza kimaisha. Anafichua kuwa kwa sababu ya ongezeko la idadi ya watu mijini, inabidi kukumbatia mifumo ya kisasa ya teknolojia ili kuzalisha chakula cha ziada. Teknolojia itasaidia kukuza chakula chenye ubora wa hali ya juu, kwa wingi katika nafasi ndogo ya ardhi. Pauline anatumia teknolojia ya kiasili ya 'Artificial Brooder' kuwatunza vifaranga dhidi ya hali mbaya ya anga ambayo inaweza kuwaangamiza kabla ya kufika sokoni. Kaunti ya Trans-Nzoia kwa ujumla hupokea kiwango kikubwa cha mvua kila mwaka na hivyo basi wafugaji kuku wamekuwa wakikadiria hasara mara nyingi kwa kuwapoteza vifaranga wao kabla ya kukomaa. Anasema aliamua kutumia aina hii ya teknolojia baada ya kubaini kuwa wakazi wengi wanapendelea kuwafuga kuku badala ya ng'ombe wa maziwa au mbuzi. [caption id="attachment_185972" align="alignnone" width="1792"] Pauline Sambu kutoka Kituo cha Kibiashara cha Tuigoin, Kaunti ya Trans-Nzoia, akilisha baadhi ya kuku wake waliokomaa na tayari kuuzwa Februari 27, 2026. PICHA|RICHARD MAOSI[/caption] “Hii ni kwa sababu kuku hawahitaji sehemu kubwa ya kukaa na pia mahitaji yao ya kila siku ni machache. Aina hii ya teknolojia ni nyepesi kwani hushirikisha matumizi ya vyungu vya kawaida ambavyo vimewekewa mashimo sehemu za kando,” anaeleza. Vifaranga hupendelea joto la kutosha hasa katika wiki ya kwanza, ambapo nyuzi joto zinapaswa kuwa kati ya 95–100°F (35–38°C). “Chungu hujazwa makaa na mashimo yenyewe hutumika kusambaza joto kwa vifaranga. Ni rahisi kutambua kama joto linawatosheleza ama la. Joto linapokua kali utawaona vifaranga wakipanua midomo pia hutanua mbawa zao na kuachiana nafasi. Ukiona hivyo fungua madirisha kwa muda mpaka wawe kwenye hali ya kawaida,” anasema. Anasema aliamua kutumia aina hii ya mfumo kwani gharama ya kununua chombo cha kisasa cha kufugia vifaranga almaarufu ‘brooder’ huwa ni ghali. Pili, wakulima wengi hawana uwezo wa kujinunulia vyombo vya kisasa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kwa sababu hawajafikiwa na uunganishaji wa stima. “Kwa kuzingatia kiwango sahihi cha nyuzi joto, vifaranga huchukua muda mfupi kabla ya kukomaa,” asema. Vifaranga wa kuanzia wiki mbili huuzwa Sh200 na wale chini ya wiki moja huuzwa Sh100. Pauline anatunza aina nne ya vifaranga wa kisasa ambao ni Sasso, Rainbow Rooster, Kuroiller na kuku aina ya chotara. Kwa ushirikiano na akina mama wengine watatu ambao pia wamejitosa kwenye ukulima huu, wao huagiza vifaranga kutoka Jinja, Uganda na eneo la Namanga. Anatoa ushauri kwa wakulima ambao wanalenga kujitosa kwenye biashara ya ufugaji wa vifaranga kwanza wanunue ndege wao kutoka kwa muuzaji aliyeidhinishwa na serikali. "Na kwa wale wenye kipato kidogo watumie uvumbuzi wa nyumbani kama huu ambao ni faafu kibiashara. Uvumbuzi utainua ukuaji wa viwanda vinavyohusika na uchakataji wa chakula pia kuimarisha pato la kitaifa.” Kadhalika, anasema kuwa wao hutumia malighafi ya kawaida yanayopatikana kwenye mazingira yao.