Bodaboda amshtaki Gavana Otuoma akidai alimpiga teke sehemu nyeti na kumuumiza

MWENDESHA piki piki almaarufu boda boda anayedai alitandikwa teke sehemu nyeti na Gavana wa Busia Paul Otuoma anaomba mahakama kuu imwagize amlipe fidia ya Sh100 milioni kutokana na majeraha aliyopata. Mbali na ombi la kumtaka Bw Otuoma amlipe fidia, Bw Yusuf Suleiman Hamisi anaomba mahakama kuu iamuru kwamba Gavana Otuoma hafai kuhudumu katika afisi ya umma kutokana na utovu wa nidhamu. Pia, anaomba mahakama kuu imwagize Spika wa Bunge la Kaunti ya Busia aanze mchakato wa kumtimua mamlakani gavana huyo kwa sababu ya utovu wa nidhamu. Bw Hamisi amesema kwamba Bw Otuoma alimtandika teke ya sehemu nyeti bila sababu. Mlalamishi ameeleza mahakama kwamba walikuwa wamepiga foleni kupokea mbegu ambazo gavana huyo alikuwa anawagawia wakazi wa eneo la Funyula. Mahakama ilielezwa kwamba “mlalamishi hakuzua vurugu zozote na ameshangaa sababu ya gavana kumvamia na kumwumiza pasipo ukorofi wowote.” Bw Hamisi aliambia korti kwamba ilibidi atorokee Nairobi kwa kuhofia maisha yake na kupokea matibabu. Bw Hamisi anayeendelea kupokea matibabu katika hospitali kuu ya Mbagathi Nairobi alieleza Mahakama kuu ya Milimani kwamba hajui ikiwa majeraha aliyopata yaliathiri nguvu zake za kiume. Bw Hamisi alimweleza Jaji Bahati Mwamuye kwamba baada ya kujeruhiwa na Bw Otuoma, alinyimwa matibabu katika hospitali ya Sio Port hata ikabidi asafiri hadi Bungoma kupokea matibabu. Mbali na matibabu, mlalamishi anadai alinyimwa Fomu ya P-3 na Polisi. Mbali na mahangaiko hayo, Bw Hamisi alisema alitekwa nyara na wanaume wanne waliokuwa wamebeba silaha hatari akitoka hospitali Bungoma. “Bw Hamisi alitoroka na kusafiri hadi Nairobi ambapo alilalazwa hospitali ya Mbagathi ambapo anaendelea kupokea matibabu,” wakili Danstan Omari anayemwakilisha alimweleza Jaji Mwamuye. Jaji huyo alifahamishwa kwamba Bw Hamisi anahofia maisha yake sawia na wakili wake. Akijibu swali la Jaji Mwamuye sababu ya kutopeleka kesi hiyo Mahakama kuu ya Busia, Bw Omari alisema ushawishi wa mshtakiwa ni mwingi na “mlalamishi pamoja naye (Omari) wanahofia maisha yao.” Jaji huyo alimwagiza Bw Omari amkabidhi nakala za mashtaka Bw Otuoma na washtakiwa wengine watatu. Mahakama imeorodhesha kesi hiyo kusikizwa Aprili 21, 2026. Pia alimwamuru Bw Otuoma awasilishe tetezi zake.