KWA NDOMO, MALINDI AJUZA aliyeheshimika kwa kupenda dini, alipatwa na aibu ya mwaka alipofumaniwa akiiba sadaka watu wakifunga macho kuomba. Shughuli kanisani zilisitishwa kwa muda pale mmoja wa waumini alipofungua macho katikati ya maombi na kumpata nyanya huyo akiwa ameinama madhabahuni huku akishika kikoba cha sadaka akichomoa manoti. Alipiga nduru ya ‘mwizi’ na kumfanya pasta kukatiza maombi ghafla. Alipofumbua macho pia aligutushwa na alichokiona mbele yake. Nyanya alikuwa bado kainama akihesabu manoti. Kuona hilo, nyanya alishtuka. Kutokana na aibu na haya, aliinua mikono yake miwili juu huku akitazama mbele ya madhabahu. Kisha alitamka: “Pasta niombee. Ni shetani tu ndiye hunidanganya. Si leo tu. Tangu niingie katika hii kanisa nimekuwa nikiiba sadaka kila mnapofunga macho. Nisameheni. Sitorudia tena,” akasema ajuza huyo kwa sauti.