ANTHONY Kinoti Mugambi aliponunua ekari mbili mwaka 2003 katika kijiji cha Kathuura, Kiagu, Central Imenti, Kaunti ya Meru, hakujua wakati mmoja hatua hiyo ingegeuka kuwa jukwaa litakalofaa nchi ya Kenya. Wakati huo ekari moja ilikuwa ikiuzwa Sh80,000 eneo hilo ambalo ni jangwa na nusu-jangwa (ASAL). Aidha, ni sehemu yenye miamba na joto kali, na linalozalisha chakula msimu wa mvua pekee. Akiwa mhandisi wa masuala ya mawasiliano, alianza kulima mahindi na maharagwe kwa minajili ya kukithi familia yake mahitaji muhimu ya kimsingi huku akitegemea mvua isiyotabirika. Hata hivyo, Kinoti aliendelea kununua ardhi na kufikia 2012 alikuwa na ekari 15. Leo hii, anamiliki ekari 50 ambapo 20 zimepandwa matunda aina ya pitaya, maarufu kwa Kiingereza kama dragon fruit , yanayostawi maeneo kame. “Ni matunda yenye thamani na faida tele kimapato na kiafya,” Kinoti anasema. Shamba lake linalojulikana kama Gravity Farms , sasa ni ngome ya ukuzaji pitaya nchini. Aidha, ni bustani mithili ya mabustani ya matunda Misri. [caption id="attachment_186033" align="aligncenter" width="300"] Anthony Mugambi (kulia), mkulima kutoka Kaunti ya Meru, aaonyesha dragon fruit anayolima pamoja na mkulima mwenzake Japhet Mutugi wakati wa Maonyesho ya Kalro Makala ya Nne ya Open Week Exhibition Kabete, Kiambu Februari 27, 2026. Picha|Sammy Waweru [/caption] Wazo la kulima pitaya lilianza alipozuru China mapema miaka ya 2000. “Niliona tunda la waridi na baadaye nikagundua ni dragon fruit,” anaelezea. Bei yake ya dola 10 (thamani ya Amerika) ilimshangaza. Aliporudi Kenya alifanya utafiti na kubaini ni mmea wa jamii ya cactus unaostahimili ukame. Mwaka 2012, kulingana na Kinoti alianza majaribio kwa kupanda mbegu. Ziliota lakini ‘zilikufa’ kutokana na maji mengi. Anasema alijifunza na kujaribu tena, na baada ya miaka minane, alipata mavuno ya kwanza 2020. Mimea michache tu ndiyo ilizaa, na minne ikawa msingi wa uzalishaji. Leo hii, Kinoti analima aina nyekundu, nyeupe na njano ya pitaya. “Njano ni tamu zaidi lakini hukomaa polepole,” anadokeza. Aidha, shamba lake liko mita 900 juu ya usawa wa bahari na anatumia maji ya mvua kuendeleza zaraa, kuteka kutoka kwenye mto na pia ana hifadhi kubwa. Mwaka 2021 alisajili rasmi biashara yake na kuingilia kilimo-kibiashara baada ya kuacha kazi yake 2018. Kinoti anajivunia kuwa miongoni mwa wakulima wa kwanza kuingiza Kenya kwenye ramani ya uzalishaji pitaya duniani. Ni matunda ghali kimauzo ambapo bei ya kilo ni kati ya Sh500 na Sh2,500. Mahitaji ni makubwa, lakini anauza zaidi ndani ya nchi. “Mwanzo nataka kuhakikisha Kenya inajitosheleza kabla kuyauza nje ya nchi,” akaambia Akilimali kwenye mahojiano ya kipekee. Pia, Kinoti huzalisha miche ya dragon fruit ambapo kwa mwezi hugonga miche 100,000. [caption id="attachment_186034" align="aligncenter" width="300"] Matunda ya dragon yaliyolimwa na Anthony Mugambi, mkulima kutoka Kaunti ya Meru. Picha|Sammy Waweru [/caption] Mwaka huu, alizindua aina mpya ya pitaya inayojulikana kama Kika yenye ladha bora na inayodumu muda mrefu kuhifadhi. Kilimo cha matunda hayo ya jangwani kimebuni nafasi za ajira kwa watu 10. Isitoshe, thamani ya ardhi Kijiji cha Kathuura, Imenti Central imeongezeka kutoka Sh80, 000 ekari mwaka wa 2003 hadi zaidi ya Sh500, 000 kwa sasa. Mkulima huyu anakiri uwepo wa changamoto, ikiwemo uelewa mdogo wa soko. “Kilimo ni safari ndefu, si mbio fupi,” anaelezea baadhi ya mambo aliyojifunza kupitia kilimo-biashara anachoendeleza. Anaamini Kenya inaweza kuwa mzalishaji mkubwa duniani wa dragon fruit katika miaka ijayo. Kimataifa sekta ya tunda hili ina thamani ya mabilioni ya dola, huku Vietnam ikiongoza uzalishaji na mapato makubwa kila mwaka. Kinoti anaona fursa kubwa kwa Kenya kutokana na ardhi kubwa isiyotumika kikamilifu. Anasisitiza umuhimu wa mbinu bora za kilimo, ikiwemo matumizi ya mbolea za asili kama samadi ya ng’ombe, mbuzi na kondoo. Hali kadhalika, anashauri wakulima wapya kuwa wavumilivu na kuwekeza katika maarifa. Licha ya changamoto alizopitia, anaamini ndoto yake itatimia kuona Kenya ikiongoza dunia katika uzalishaji wa pitaya sawa na matunda mengine kama avocado, maembe na ndizi, ikiwa uwekezaji utaongezeka na soko kuimarishwa.