MAJANGILI wanazidi kuwa jasiri kufuatia shambulizi lililotekelezwa jana adhuhuri, saa chache baada ya Naibu Inspekta Jenerali wa Polis, Eliud Lagat kuongoza kikao cha usalama eneo la Tigania Mashariki, Meru, na kusababisha kifo cha mtu mmoja. Bw Lagat aliongoza kikao cha usalama eneo la Kandebene, kilichoshirikisha maafisa kutoka kaunti za Isiolo na Meru, ambapo aliapa kukomesha ujangili eneo hilo. Chifu wa Buuri John Mamira, alisema majangili hao sugu walishambulia punde baada ya mkutano kukamilika, wakamuua mtu mmoja na kumjeruhi mwingine mguuni eneo la Ntangilia. Idadi isiyojulikana ya ng’ombe waliibiwa. Katika mkutano huo wa usalama uliohudhuriwa na Mbunge wa Tigania Mashariki, Mpuru Aburi, Bw Lagat aliwaagiza majangili kutekeleza vitisho vyao vya kushambulia mbele yake. “Nimepokea habari kuwa majambazi wanadhihaki na kutishia kushambulia baada ya mkutano wetu wa usalama. Watakumbana na hamaki ya timu ya GSU nitakayoacha,” alisema Bw Lagat. Aliagiza kamanda wa GSU anayesimamia oparesheni kuchukua usukani na kuelekeza shughuli za kiusalama eneo hilo. “Tutatumia mbinu zilezile tulizotumia kuangamiza ujangili Bonde la Ufa Kaskazini, kurejesha utulivu Meru. Hatuwezi kuruhusu majambazi kuzurura huru na kuiba mali kutoka sehemu yoyote nchini. Operesheni zinaendelea Laikipia na Samburu na hivi karibuni tutakuwa Isiolo na Meru. Majangili wataona cha mtema kuni,” alisema. Shambulizi la Jumanne ni miongoni mwa misururu ya mashambulizi ambayo kufikia sasa yamewaua watu sita Tigania Mashariki katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita. Malalamishi yamezidi kuongezeka miongoni mwa wachungaji na viongozi kuhusu mashambulizi ya majangili ambayo yameongezeka katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita. Diwani wa Wadi ya Muthara Aurelio Murangiri, alisema ongezeko la ujangili linahusishwa na itikadi ya jadi ambapo vijana barobaro wanaotahiri kutoka jamii jirani ni sharti wathibitishe ujuzi wao wa vita kupitia uvamizi. Aidha, kero hilo limehusishwa na mabwenyenye wanaolenga wanyama ili kuwauza kimagendo. Kulingana na wanachama wa kundi la Viongozi wa Kidini Tigania Mashariki waliowasilisha malalamishi kwa afisi ya naibu kamishna wa kaunti Jumatatu, watu wasiopungua 103 wameuawa na mifugo zaidi ya 10,980 wameibiwa kutoka Meru tangu 2023.