Utaacha siasa za kumezea mate kiti cha Kindiki, Hassan Omar amuonya Joho

SIKU chache tu baada ya Rais William Ruto na Kinara wa ODM Bw Oburu Odinga kutoa wito wa kukomeshwa kwa uhasama wa kisiasa kati ya viongozi wa vyama vya ODM na UDA eneo la Pwani, Katibu Mkuu wa chama tawala Bw Hassan Omar, amejitokeza na kuanza kumshtumu Waziri wa Madini, Hassan Joho kwa kueneza siasa za kumezea kiti cha unaibu wa rais. Bw Omar alionya wanachama wa ODM kwa kuendeleza siasa za kushawishi kundolewa kwa Naibu wa Rais Prof Kithure Kindiki katika uchaguzi mkuu wa 2027 na kurithiwa na Waziri Joho. ”Huwezi danganya watu milele, ati mtoto wa kipwani awe Naibu wa Rais. Wanajua hawajafanya kazi, wanajua siasa zao ni za hamasa na hawataki watu waongee kuhusu uongozi wao sababu walishindwa. Wakati ule mwingine walikuwa wanapigana na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta wakahuriwa na kupita wakati wa uchaguzi mkuu. Lakini hatutahadaiwa tena,” alisema Bw Omar. Alionya Wapwani dhidi ya kueneza siasa za unaibu wa urais na ukabila. “Mimi niingie debeni, niko na Prof Kindiki na Bw Joho lakini nimchague Bw Joho kuwa naibu wa rais 2027 sababu ni Muislamu mwenzangu, sijui tumetoka Kibokoni pamoja?” alisema. Bw Omar alisema kuwa UDA itasimamisha wagombeaji katika viti vyote vya kisiasa, akisisitiza kuwa chama hicho kinasalia na msimamo wa ushindani wa kisiasa. licha ya shinikizo zinazoendelea za kuunganisha viongozi. Vile vile alisema hatokubali kumwachia Gavana wa Mombasa Bw Abdulswamad Nassir kiti hicho wakati wa uchaguzi mkuu wa 2027. Bw Omar ambaye atawania tena kiti cha ugavana wa mara ya tatu wakati wa uchaguzi mkuu wa 2027 alisema licha ya uhusiano wa serikali ya ushirikiano (broad based government) kati ya UDA na ODM hatomwachia Bw Nassir kiti hicho. Alisema atamenyana na Bw Nassir ambaye alimshtumu kwa kukosa kufanya miradi yoyote ya maendeleo miaka mitatu tangu aingilie mamlakani. “Tutaendelea na ushirikiano lakini lengo langu ni kuhakikisha Bw Nassir hapati ugavana, amehadaa wakazi wa Mombasa. Kuwe na ushirikiano wowote, kuwe na broad based government yoyote lakini tutampeleka kwao nyumbani,” alisema Bw Omar. Alisema UDA haitakubali mpango wowote wa kutenga maeneo ya kisiasa (zoning) kwa wagombea wa ODM. “Hawezi kuendelea na uongozi wa huu mji. Gavana Nassir amekuwa na mzaha, hata ndugu yetu Bw Joho alikuwa na afadhali. Huyu kazi yake kwenda sherehe za wajomvu na wachangamwe. Haiwezekani tukafika hapa katika mji wetu,” alisema Bw Omar. Alisema viongozi wa UDA watampigia debe Rais Ruto kupata muhula wa pili lakini viongozi wengine watamenyana kati ya ODM na chama tawala. Hata hivyo, naibu mkurugenzi mkuu wa kampeni na uchaguzi wa ODM, Dkt Noah Akala alisema Bw Omar ameanza kubabaika kuhusu uchaguzi mkuu. “Sielewi ni kwa nini anababaika. Ameanza kuropokwa hata kabla kamati kamati ambayo viongozi wa vyama vya ODM na UDA wakiongozwa na Bw Oburu na Rais Ruto kuanza kujadili masharti ya makubaliano yanayoweza kufikiwa. Sijui anazungumza kwa mamlaka gani,” alisema Dkt Akala.