WAISLAMU kote nchini Kenya wanajiandaa kushuhudia rasmi mwandamo wa mwezi wa Shawwal, unaobainisha mwisho kamili wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Tayari, Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, ametangaza leo Ijumaa kuwa sikukuu kuadhimisha Idd-ul-Fitr. Bw Murkomen alitoa tangazo hilo kupitia notisi maalum ya gazeti rasmi la serikali Machi 18, 2026. “Waziri wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa ametangaza kwamba, Ijumaa Machi, 20 2026, itakuwa siku ya mapumziko ya umma kuadhimisha Idd-ul-Fitr,” ilisema notisi hiyo. Idd-ul-Fitr huashiria kumalizika kwa Ramadhani, mwezi unaotengwa kwa ajili ya kufunga, sala na tafakari ya kiroho. Mwaka huu, Waislamu nchini Kenya walianza kuadhimisha Ramadhani Februari 19 baada ya kuthibitishwa kwa mwandamo wa mwezi hapa nchini. Sherehe hii haiashirii tu mwisho wa mfungo bali pia huwakilisha shukrani, mwanzo mpya na umoja ndani ya jamii ya Kiislamu. Familia hukusanyika kwa chakula, hubadilishana zawadi na kufanya matendo ya ukarimu, jambo linaloimarisha mshikamano wa kijamii na huruma. Mwaka huu, waumini wa Kiislamu na Kikristo duniani kote walianza kwa pamoja kipindi muhimu cha kufunga, kujitafakari na kujichunguza siku moja, ingawa chimbuko la ibada hizo ni tofauti hali iliyoshuhudiwa mara ya mwisho takriban miaka 32 iliyopita. Wakristo walianza kipindi cha Kwaresima siku ya Jumatano ya Majivu tarehe Februari 18, huku Waislamu wakianza mwezi mtukufu wa Ramadani siku hiyo hiyo baada ya kuonekana kwa mwezi mwandamo mpya Jumanne, tarehe 17 Februari. Kwa mujibu wa notisi iliyotolewa na Kaimu Kadhi Mkuu Sukyan Hassan Omar, Kamati ya Kitaifa ya Kuandama Mwezi ilikutana katika Mahakama ya Kadhi, Upper Hill, Nairobi kuanzia saa 12 jioni hadi saa 3 usiku kupokea na kuthibitisha taarifa za kuonekana kwa mwezi mwandamo.