NAIBU Rais Kithure Kindiki alirudi katika eneo la Pwani na kukutana na mvutano wa kisiasa kati ya wanasiasa wa chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) na kile cha Orange Democratic Movement (ODM) wanaomenyania nafasi yake wakati wa uchaguzi ujao. Waziri wa Madini na Uchumi wa Bahari Bw Hassan Joho, ambaye anamezea mate nafasi hiyo, amekuwa akiwarai viongozi wa Pwani kumuunga mkono kabla ya mazungumzo ya UDA-ODM. Hata hivyo, wenzake wa UDA wakiongozwa na Waziri Salim Mvurya, Katibu Mkuu wa chama tawala Bw Hassan Omar walimuonya dhidi ya kupanua mamlaka yake kupita kiasi ndani ya serikali pana. Prof Kindiki aliwahimiza wakazi wa pwani kumrejesha mamlakani Rais William Ruto kwa muhula wa pili, akitaja rekodi ya maendeleo katika eneo hilo. “Ninawasihi mmrudishe Rais Ruto kwa muhula wa pili. Lakini kwa hivyo viti vingine vya kisiasa mtamenyana kati ya UDA na ODM sababu sote ni ndugu. Dkt Ruto ndiye Rais wa kwanza aliyesaidia kuunganisha taifa hili. Na hata kabla ya kifo cha kiongozi wa ODM Raila Odinga, wawili hao walikuwa wameafikiana kuunganisha UDA na ODM. Sasa lazima tusonge mbele pamoja,” alisema. Naibu Rais alisisitiza kuwa ODM na UDA ni mrengo mmoja. Hata hivyo aliwahimiza wanachama wa ODM kuimarisha chama chao dhidi ya mgogoro unaotokota. “UDA pia tuimarishe chama chetu kiwe na nguvu ili tusonge mbele kama kitu kimoja. ODM msiruhusu mpasuko ndani ya chama chenu. Tunataka kuwa na vyama viwili imara,” alisema, akitaja ushindani wa viti vya kisiasa kati ya vyama hivyo viwili kama mapambano ya kirafiki kati ya ndugu. Akiandamana na Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro na wabunge Kenneth Tungule (Ganze), Owen Baya (Kilifi Kaskazini) na Aisha Jumwa (Mwenyekiti, Kenya Roads Board), Naibu wa Rais alitangaza kuwa chama cha Pamoja African Alliance (PAA) kimeamua kuunga UDA. “Mbunge wa Ganze Kenneth Tungule, Gonzi Rai wa Kinango na Kenga Mupe wa Rabai wote walichaguliwa kupitia PAA, kilichokuwa kikiongozwa na Spika Amason Kingi. Lakini wameamua kujiunga na UDA kuimarisha chama chetu. Spika Kingi, Tungule, Rai na Mupe wote sasa wako UDA,” alisema Prof Kindiki. Wiki iliyopita, Spika Kingi, ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa PAA, alitangaza kuwa chama hicho hakitashiriki tena katika kinyang’anyiro cha kisiasa badala yake kitaunga UDA. Spika Kingi alisema uamuzi huo ulifikiwa baada ya mashauriano ya kina kati yake na Rais Ruto pamoja na viongozi wa mashinani wa PAA. Mbunge wa Ganze, ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa PAA, alithibitisha chama hicho kimeunga UDA. “Niliwahi kuwa Katibu Mkuu wa PAA, lakini sasa tumejiunga na UDA. Mnamo 2027 nitapigania kiti changu kwa tiketi ya UDA. Tuko sasa katika serikali jumuishi. Najua mazungumzo yanaendelea, lakini nataka niseme wazi kuwa hakuna mazungumzo kuhusu kiti cha Unaibu Rais. Wanaokuja kwa mazungumzo waepukane na kiti hicho,” alisema Bw Tungule. Bi Jumwa alisema hakuna mazungumzo kuhusu nafasi ya Naibu Rais katika mazungumzo ya UDA-ODM.