WALINZI wa kibinafsi nchini huenda wakakabiliwa na ushindani mkali au hata kupoteza ajira katika baadhi ya taasisi za umma na kibinafsi iwapo Bunge litapitisha hoja inayopendekeza wanaohitimu kutoka Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) watwae kazi hizo. Hoja hiyo iliyowasilishwa bungeni na Mwakilishi wa Kike wa Kilifi Gertrude Mbeyu inalenga kuwapa wanaohitimu NYS ajira rasmi pamoja na masharti yaliyo wazi ya kazi, ikiwemo mishahara na mfumo wa kupandishwa vyeo. Hata hivyo, kipengele kinachopendekeza wahitimu wa NYS kutengewa kiwango maalum cha nafasi za ulinzi katika taasisi za umma na kampuni za kibinafsi za ulinzi kinamaanisha kuwa baadhi ya walinzi wa sasa wanaoajiriwa na kampuni hizo wanaweza kubadilishwa na wahitimu wa NYS. “Kuna haja ya kuwa na mkakati wa usawa unaochochea ajira kwa vijana kupitia kushirikisha wanaohitimu NYS kwa utaratibu uliopangwa huku tukilinda nafasi za kampuni za kibinafsi za ulinzi kuendelea kufanya kazi na kushirikiana na taasisi za serikali,” inasema sehemu ya hoja hiyo. Ikiwa hoja itapitishwa na serikali kutekeleza mapendekezo yake, wabunge wanataka serikali ya kitaifa kuweka vigezo vya kuamua mfumo wa kugawa nafasi za utoaji wa huduma za ulinzi kati ya wahitimu wa NYS na kampuni za kibinafsi. Hii ina maana kuwa kutakuwa na idadi maalum ya nafasi za walinzi zitakazotengewa vijana wanaohitimu NYS katika taasisi za umma na hata baadhi ya mashirika ya kibinafsi. Hoja hiyo pia inataka serikali kubuni utaratibu wa wazi wa kuajiri, kupeleka kazini na kuweka masharti ya huduma kwa wahitimu wa NYS, ikiwemo mishahara, mafunzo na nafasi za kupanda vyeo kazini. Ikiwa mapendekezo hayo yataidhinishwa, wizara, idara na mashirika ya serikali pia yatahitajika kuwapa kipaumbele wahitimu wa NYS wanapoongeza walinzi katika majengo yao. Bi Mbeyu anasema taasisi nyingi za serikali zimekuwa zikitegemea kampuni za kibinafsi za ulinzi kusaidia maafisa wa usalama wa serikali, jambo ambalo limekuwa likigharimu serikali fedha nyingi kila mwaka. Hatua hiyo, hata hivyo, inaweza kuathiri vibaya kampuni za kibinafsi za ulinzi ambazo kwa sasa zinatoa huduma katika majengo mengi ya serikali na taasisi za ki binafsi kote nchini. Kulingana na takwimu za Wizara ya Usalama wa Ndani, kuna zaidi ya kampuni 2,000 zilizosajiliwa za ulinzi nchini ambazo kwa pamoja zinaajiri zaidi ya walinzi milioni 1.3. Kampuni hizo mara nyingi husaidia maafisa wa usalama kufanya doria katika maeneo ambako polisi ni wachache. Katika mikusanyiko ya umma au maandamano, walinzi hao pia hushirikiana na maafisa wa usalama kudhibiti umati na kuhakikisha usalama wa washiriki. Serikali imekuwa ikianzisha mipango mbalimbali ya kuwapa wahitimu wa NYS ujuzi wa kupata ajira katika sekta muhimu kama vile kilimo, ujenzi na usalama. Hoja hiyo inasema wahitimu wa NYS tayari wana mafunzo ya msingi kuhusu nidhamu, uelewa wa masuala ya usalama, huduma kwa umma na kukabiliana na dharura, jambo linalowafanya kufaa kuajiriwa katika taasisi za serikali. “Bunge hili linataka serikali ya kitaifa kuunda na kutekeleza sera na miongozo itakayosaidia wizara, idara na mashirika ya serikali kuwapa kipaumbele wahitimu wa NYS katika utoaji wa huduma za ziada za usalama katika taasisi za umma,” inasema hoja hiyo. Hoja hiyo pia inalenga kusaidia serikali kupunguza mzigo wa kukosa ajira kwa maelfu ya vijana nchini. Chini ya Katiba ya Kenya, hasa Kifungu cha 55, serikali inatakiwa kuweka hatua maalum, ili kuhakikisha vijana wanapata mafunzo, ajira na fursa za kushiriki kikamilifu katika maisha ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ya taifa. Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa takriban vijana 18,000 huhitimu kutoka NYS kila mwaka. Baadhi yao hujaribu kujiunga na vikosi kama polisi au jeshi, huku wengine wakirejea vijijini bila ajira ya kudumu. Mwezi uliopita, Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku aliambia Bunge kuwa serikali inapanga kuongeza mara mbili idadi ya vijana wanaojiunga na NYS katika mwaka ujao wa kifedha. Hata hivyo, alionya kuwa mpango huo unaweza kuchelewa kutokana na upungufu wa fedha baada ya wizara kuomba Sh23 bilioni lakini ikatengewa Sh10 bilioni pekee katika bajeti. NYS ilianzishwa mwaka 1964 kwa lengo la kuwafunza vijana kuhudumia taifa na kushiriki katika miradi ya maendeleo ya kitaifa. Huduma hiyo husajili vijana kwa kujitolea wenye umri wa kati ya miaka 18 na 24, ambao hupitia mafunzo ya msingi ya kijeshi kwa miezi sita katika chuo cha NYS kilichoko Gilgil kabla ya kupelekwa katika kambi mbalimbali za huduma kote nchini. Baada ya mafunzo hayo, vijana hushiriki katika shughuli za kujenga taifa kama ujenzi wa barabara, kilimo cha kibiashara, uhifadhi wa mazingira na utoaji wa huduma za usalama katika taasisi mbalimbali za umma.