SERIKALI ya Israeli imedai kuwa imemuua Waziri wa Ujasusi wa Iran, Esmail Khatib, katika mashambulizi yaliyofanywa usiku wa kuamkia Jumatano. Haya yanajiri huku Tehran ikifanya misa ya pamoja ya kuwazika maafisa wake waliouliwa wakiwemo Ali Larijani aliyekuwa mkuu wa usalama wa taifa, kamanda wa kikosi cha Basij Gholamreza Soleimani pamoja na mabaharia. Kuuawa kwa Esmail Khatib ni pigo jingine kwa Jamhuri hiyo ya Kiislamu katika vita hivyo vilivyoanza zaidi ya wiki mbili zilizopita. Mashambulio yaliyomuua waziri huyo yalifanywa saa chache baada ya vyombo vya habari vya serikali ya Iran kuthibitisha juu ya kuuwawa kwa maafisa wake wa ngazi za juu wa usalama Ali Larijani na jenerali Gholam Reza Soleimani. Hapo jana, Umma ulikusanyika katika uwanja wa Enghelab mjini Tehran mamia wakihudhuria mazishi ya viongozi hao wakiwa wamebeba picha za viongozi wao wa juu kuanzia muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ruhollah Musavi Khomeini, Ayatollah Ali Khamenei na Mojtaba Khamenei na kupeperusha bendera huku wakijipiga vifua kama heshima kwa waliouwawa na mashambulizi ya Israeli. Ali Larijani alitazamwa kwa kiasi kikubwa nchini Iran kama mmoja wa watu wenye usemi na aliyekuwa mtu wa karibu zaidi na kiongozi wa Juu aliyetangulia kuuwawa kwenye vita hivyo, Ayatollah Ali Khamenei na mwanawe Mojtaba Khamenei aliyerithi uongozi. Urusi imeonyesha kuchukizwa na mauaji ya Larijani, msemaji wa rais Vladmir Putin Dmitry Peskov alisema nchi hiyo inalaani mashambulio ya kuwalenga viongozi wa Iran. Mashambulizi ya Israeli yameendelea pia kutikisa mji mkuu wa Lebanon Beirut, ripoti zikionyesha kwamba jengo moja la makazi liliharibiwa kabisa katika mji wa Bachoura na majengo mengine mawili pia yalilengwa katika eneo la Beirut ambako takriban watu sita waliuwawa. Wakati huo huo rais Donald Trump amesema Amerika huenda ikaliacha suala la Usalama wa Mkondo wa Hormuz, kwa mataifa yaliyokataa wito wake wa kutuma meli za kivita kama Uingereza.