MIKUTANO ya wajumbe wa kitaifa ya vyama vya kisiasa nchini mara nyingi huwa mahali ambapo nyota za kisiasa huzaliwa huku nyingine zikizimika ghafla. Katika historia ya siasa za Kenya, mikutano hii imekuwa na nguvu kubwa ya kuamua mustakabali wa vyama na viongozi wake. Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kilichoanzishwa na marehemu Raila Odinga sasa kinajikuta katika mvutano mkubwa wa uongozi kufuatia kifo cha kiongozi huyo Oktoba mwaka jana. Kwa sasa chama kinaongozwa kwa muda na kakake mkubwa, Dkt Oburu Oginga, huku kikijiandaa kufanya mkutano mkuu wa wajumbe wiki ijayo. Hata hivyo, mkutano huo tayari umeibua mvutano mkali ndani ya chama. Katika historia ya siasa za Kenya, mikutano ya aina hii imewahi kubadilisha mkondo wa uongozi wa vyama au kuvisambaratisha. Mfano ni tukio la mwaka 2002 wakati wa muungano wa vyama vya Kanu na NDP katika uwanja wa Kasarani. Wakati huo, marehemu Profesa George Saitoti alikuwa akinuia kubaki katika wadhifa wa makamu mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha Kanu, nafasi ambayo ingeweza kumweka mstari wa mbele kumrithi Rais Daniel arap Moi aliyekuwa akimaliza muhula wake wa mwisho madarakani. Hata hivyo, Rais Moi alitoa tangazo lililoshangaza wengi alipofuta wadhifa wa makamu mwenyekiti wa kitaifa na kuanzisha nafasi nne za makamu wenyekiti badala yake, hatua iliyomshusha hadhi Profesa Saitoti. Jaribio la Saitoti kupinga hatua hiyo halikufua dafu baada ya Moi kumkemea hadharani akisema: “Nyamaza, Profesa! Kama jina lako haliko kwenye orodha, basi haliko.” Baada ya kukemewa, Profesa Saitoti alilazimika kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho na kutoa hotuba fupi iliyobaki kukumbukwa katika historia ya siasa za Kenya. “Inafika wakati ambapo taifa ni muhimu kuliko mtu binafsi. Kwa kuzingatia hilo na baada ya mashauriano, nasema sitawania wadhifa wowote,” alisema mbele ya wajumbe wa Kanu. Sasa hali sawa na hiyo inaonekana kujitokeza ndani ya ODM. Chama hicho kimegawanyika katika makundi mawili yanayovutana kuhusu mkutano mkuu wa wajumbe unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo. Kundi moja linaongozwa na Dkt Oburu Oginga ambaye kwa sasa ni kiongozi wa muda wa chama. Kundi hilo linaunga mkono kufanyika kwa mkutano rasmi wa wajumbe katika viwanja vya Jamhuri jijini Nairobi. Hata hivyo, kundi pinzani linaloongozwa na Katibu Mkuu Edwin Sifuna, linalojulikana kama Linda Mwananchi, limetangaza kuwa litafanya mkutano wake tofauti wa wajumbe jijini Nairobi. Mwenyekiti wa ODM na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga amesisitiza kuwa chama kitafanya mkutano mmoja tu wa wajumbe kulingana na katiba ya chama. “Kutakuwa na mkutano mmoja tu wa wajumbe wa ODM. Njia za kuitisha mkutano huo zimetajwa katika katiba ya chama. Watu wako huru kufanya mikutano ya kisiasa au mikutano ya kijamii, lakini mkutano wa wajumbe wa ODM utafanyika katika viwanja vya Jamhuri,” alisema. Kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohammed pia alisisitiza kuwa mkutano huo utaendelea kama ulivyopangwa. “Watu watatu au wanne wakipinga, huwezi kusema chama kimekumbwa na vurugu. Baadhi ya watu hawa waliangamiza vyama vingine zamani. Hatutaruhusu waharibu ODM. Waje tukutane nao katika mkutano wa wajumbe,” alisema. Kwa upande wake, Gavana wa Siaya James Orengo, ambaye ni mmoja wa viongozi wa kundi la Linda Mwananchi, amesema kundi hilo halitahudhuria mkutano uliopangwa na mrengo wa Dkt Oginga. “Tarehe Machi 27 tutafanya mkutano wa wajumbe wa wananchi hapa Nairobi, na mwaliko wa mkutano huo utatangazwa kwa wakati ufaao,” alisema Orengo. Mhadhiri na mchambuzi wa siasa Profesa David Monda, ameonya kuwa mvutano huo unaweza kuwa na athari kubwa kwa chama hicho. “Athari zake ni kwamba mkutano wa wajumbe wa ODM unaweza kukitumbukiza katika mzozo mrefu wa kisheria mahakamani ambao unaweza kuwa na madhara makubwa. Pia kuna uwezekano wa chama kugawanyika zaidi na kusababisha wanachama wengi kuhama ODM kuelekea vyama vingine kadri uchaguzi wa 2027 unavyokaribia,” alisema Profesa Monda. Aliongeza kuwa hali hiyo inafanana na mikutano ya wajumbe ya zamani iliyogubikwa na vurugu za kisiasa.