Mataifa ya Mashariki ya Kati yaadhimisha Idd huku mapambano kati ya Iran, Amerika na Israeli yakichacha

MATAIFA ya Mashariki ya Kati kama vile Saudia Arabia wanasherehekea sikukuu ya Idd mashambulizi yakiendelea kati ya Iran, Israeli na Amerika. Sikukuu ya Idd katika Mataifa ya Ghuba zitafanyika katika misikiti ya kawaida badala ya umati wa watu kukusanyika viwanjani kama ilivyo ada, hiyo ikiwa ni tahadhari tu kutokana na mashambulizi yanayofanywa na Iran kwa mataifa hayo. Wapalestina katika Ukanda wa Gaza nao walikusanyika kuadhimisha sikukuu ya Idd inayoashiria mwisho wa mwezi wa mfungo wa Ramadan. Wakiwa wamedhamiria kukiondoa kiwingu kilicholetwa na vita katika ukanda huo, wazazi katika eneo la Khan Younis walikusanyika kuoka biskuti kusherehekea na watoto wao ambao maisha yao yameathirika vibaya na vita. Huku mapigano makali yakiwa yamepungua huko Gaza kutokana na makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa, Israeli imekuwa ikifanya mashambulizi ya hapa na pale kila kukicha. Nchini Iraq katika mji wa Erbil nako, maandalizi ya sherehe hizo yalifanyika ila kwa kasi ndogo huku wasiwasi wa usalama ukiwa umewagubika raia kutokana na vita vya Iran, Amerika na Israeli. Wamiliki wa maduka katika mji huo wanasema mazingira yamebadilika katika sherehe za mwaka huu ikilinganishwa na sherehe za mwaka jana. Licha ya wasiwasi ulioko, masoko yamesalia wazi huku familia zikiendelea kufanya ununuzi kwa ajili ya sherehe hizo za Idd. Tangu kuanza kwa vita vya Iran mnamo Februari 28, Iraq imeshuhudia mashambulizi kadhaa yakiwemo ya droni na makombora yaliyolenga kambi za kijeshi, miundo mbinu ya mafuta na maeneo mengine. Nako nchini Afghanistan waumini wa Kiislamu waliadhimisha sikukuu ya Idd kwa sala katika msikiti wa Sha-Do Shamshira. Mapema Jumatano, Afghanistan na Pakistan walitangaza usitishwaji wa mapigano yanayozidi baina ya nchi hizo mbili, siku mbili baada ya Kabul kuilaumu Islamabad kwa shambulizi la angani katika mji huo mkuu, lililosababisha vifo vya mamia ya watu. Nchi hizo mbili zilitangaza kwa pamoja kuwa zingesitisha vita kupisha sherehe za Idi kutokana na wito wa Saudi Arabia, Uturuki na Qatar. Huko Pakistan nako sikukuu hiyo iliadhimishwa Alhamis huku maelfu ya watu wakiwa wamefurika kwenye vituo vya mabasi na treni eneo la Lahore kujaribu kusafiri kuelekea maeneo ya vijijini kwa ajili ya kusherehekea na familia zao. Hali ilikuwa sawa na hiyo nchini India na Bangaldesh ambako Waislamu waliidhimisha sherehe ila sherehe za mwaka huu zimegubikwa na vita vinavyoendelea nchini Iran, ambavyo vimesababisha kuongezeka kwa bei za mafuta na gesi. Katika Mji Mkuu wa India New delhi, uhaba wa mitungi ya gesi inayotumiwa na wengi kwa mapishi, liliwalazimu wengi kutumia meko yanayotumia makaa, kuandaa vyakula vya sikukuu. Haya yanafanyika huku Iran ikitarajiwa kuadhimisha Idd leo.