Wamuthende akosa kufika kortini kuhojiwa kuhusu kesi ya kupinga ushindi wake

KESI ya kupinga matokeo ya uchaguzi mdogo wa eneo la Mbeere North umechukua mkondo mpya baada ya Mbunge Leo Wamuthende Njeru kukosa kufika mbele ya mahakama kuhojiwa, akiamua kutegemea tu hati yake ya kiapo aliyowasilisha. Hatua hiyo imeibua upinzani mkali kutoka kwa Newton Kariuki Ndwiga, ambaye sasa anataka mahakama imuondoe mbunge huyo kwa kukosa kujitokeza kujibu maswali chini ya kiapo. Kupitia timu yake ya mawakili wakiongozwa na Kiragu Wathuta na Ndegwa Njiru anasema Njeru hapaswi kuruhusiwa kushiriki katika kesi bila kusimama kizimbani kutetea madai yake. Mlalamishi anaomba mahakama iamuru kuhesabiwa upya na kuchunguzwa kwa kura katika vituo 32 kati ya 134 vilivyotumika wakati wa uchaguzi huo. Anadai kuwa kasoro katika stakabadhi za uchaguzi zinaweza kubadilisha matokeo ya mwisho iwapo zitathibitishwa. Pia, alidai kuwa idadi kubwa isiyo ya kawaida ya wapiga kura waliosaidiwa kupiga kura ilikuwa sehemu ya mpango uliomdhuru kisiasa. Hata hivyo, upande wa utetezi umepinga madai hayo vikali. Wakili Charles Mwongela, anayewakilisha Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) pamoja na maafisa wa uchaguzi, alitaja ombi la uchunguzi wa kura kama “jaribio la kutafuta makosa bila ushahidi.” Mwongela alisema mlalamishi hajabainisha kasoro zozote mahsusi katika fomu muhimu za uchaguzi zilizotumika kutangaza matokeo. Alitetea pia uadilifu wa mchakato wa uchaguzi akisema mfumo wa Usimamizi wa Uchaguzi Kenya Kenya ulifanya kazi ipasavyo, huku sajili za wapiga kura za karatasi zikitumika kama mbadala pale changamoto za kiufundi zilipojitokeza. Mahakama pia ilielezwa kuwa madai yanayomhusisha Waziri Geoffrey Ruku kwa kuingilia shughuli za vituo vya kupigia kura hayakuungwa mkono na ushahidi wowote. Kuhusu tukio la moto katika moja ya vituo vya kupigia kura, upande wa utetezi ulisema lilisababishwa na taa ya mafuta iliyotumiwa na maafisa wa uchaguzi kutoa mwanga wakati wa kuhesabu kura, ukikanusha madai kwamba lilikuwa jaribio la kuharibu vifaa vya kura. Mahakama Kuu mjini Embu inatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu ombi la kuchunguza masanduku ya kura na vifaa vya uchaguzi Machi 26, 2026. Katika hati yake ya kiapo, Ndwiga alidai kuwa uchaguzi mdogo huo ulikumbwa na kasoro nyingi na kwamba ushindi wa Njeru unapaswa kubatilishwa. Alisema baadhi ya vituo vya kupigia kura vilikumbwa na vurugu na vitisho vilivyosababisha upigaji kura kusimamishwa au kuvurugika. Aidha alidai kuwa baadhi ya wapiga kura waliokuwa wamesajiliwa walizuiwa kupiga kura au kunyimwa haki yao kupitia udanganyifu katika sajili ya wapiga kura na kutofuatwa kwa taratibu za upigaji kura.