Oburu afichua uhusiano wake na Raila

KWA zaidi ya nusu karne, Seneta wa Siaya, Dkt Oburu Oginga, alisimama imara kando ya kaka yake mdogo Raila Odinga, si kama mpinzani, si kama mshindani, bali kama mshauri mwaminifu, mkakati wa kisiasa na nguvu kimya nyuma ya ukoo wa Odinga. Katika familia nyingi za Kiafrika, mzaliwa wa kwanza hushikilia mamlaka ya kifamilia, na jaribio lolote la kupokonywa nafasi hiyo huibua migogoro mikali kama hadithi ya kibiblia ya Yakobo na Esau. Lakini kwa Dkt Oginga ambaye sasa ni Kaimu Kiongozi wa Chama cha ODM, kuwa kifungua mimba katika familia ya Jaramogi Oginga Odinga kulimaanisha jambo tofauti: alichagua uaminifu badala ya uongozi, unyenyekevu badala ya mgawanyiko. “Raila hakuwa tu kaka yangu, alikuwa rafiki yangu, rika langu, mshauri wangu, mshirika wangu wa kibiashara. Nilimheshimu kama kiongozi wangu wa kisiasa,” alisema Dkt Oginga mbele ya maelfu ya waombolezaji katika uwanja wa Nyayo. Kuanzia enzi za KANU hadi mabadiliko ya vyama vingi, Dkt Oginga alibaki nyuma ya Raila, akichukua mzigo wakati hali ilikuwa mbaya, akimkinga kaka yake, na kulinda ushawishi wa kisiasa wa familia. Katika dunia ambapo siasa hugawanya familia, uaminifu wa Dkt Oginga kwa kaka yake mdogo ni nadra na wa kipekee — udugu uliopimwa kwa miongo mingi ya mapambano, nguvu na kujitolea. Alizaliwa Oktoba 15, 1943, katika kijiji cha Sakwa, Bondo, Siaya kabla ya uhuru wa Kenya. Akiwa mwana wa kwanza wa Jaramogi, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, matarajio yalikuwa makubwa. Lakini, kama anavyosema Mzee Edwin Onyango Radier, aliyekuwa msaidizi wa Jaramogi: “Oburu alikuwa mpole, mwerevu, na mwenye hekima. Hakufuata njia ya mkwaruzano kama Jaramogi au Raila. Alikuwa mkono wa utulivu katika familia ya Odinga.” Mzee Olang’o Nyabola anaongeza: “Raila alikuwa na moto wa kisiasa, jasiri na mpambanaji. Oburu alikuwa mtulivu, mwelewa na mwenye ushawishi wa chini kwa chini. Pamoja walisaidiana vyema.” Baada ya kifo cha Jaramogi 1994, wengi walidhani Dkt Oginga angechukua usukani kisiasa katika familia. Lakini alijiondoa kwa hiari, akatangaza Raila alikuwa kiongozi bora. “Uongozi si haki ya kuzaliwa,” alisema wakati huo. “Ni suala la nani anaweza kuongoza watu kwa matumaini. Raila ana kipawa hicho, nami nitamuunga mkono milele.” Na kweli, alimsaidia Raila kwa dhati, kwa zaidi ya miongo mitatu, wakati wa kukamatwa, kupigania mageuzi, kupoteza chaguzi, na kuongoza vuguvugu la matumaini nchini Kenya. Alipokuwa Mbunge wa Bondo kwa zaidi ya miaka 20, alijulikana kwa heshima, bidii, na kujitolea kwa maendeleo ya Siaya. Alihimiza ugatuzi, usawa, na uwajibikaji, sawa na misingi ya Raila. Tangu kuzaliwa kwa ODM mwaka 2005, Dkt Oginga amekuwa mmoja wa washauri wakuu. Alifahamika kama “sauti ya busara” ndani ya chama, akiwa kiungo kati ya kizazi kipya cha vijana na wanasiasa wa kizazi cha zamani. Aliwahi kuhudumu pia kama mweka hazina wa chama na mlezi wa kisera. Kila hali ilipochacha, alikuwa na uwezo wa kutuliza kwa hekima ya kihistoria na uzoefu wa kifamilia. Dkt Oginga pia alikuwa nguzo ya familia ya Odinga. Akiwa msemaji wa familia, mara nyingi alikuwa akitoa taarifa za afya ya Raila, hata pale wasaidizi wake waliponyamaza.