Polisi katika Kaunti ya Homa Bay wameanzisha uchunguzi kuhusu kisa cha kuteketezwa kwa nyumba ya Mbunge wa Rangwe, Dkt Lilian Gogo, katika kijiji cha Kotieno, Ijumaa usiku. Nyumba hiyo iliteketezwa moto mbunge huyo akishughulikia mipango ya mazishi ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Amolo Odinga, akiwa mwanachama wa Kamati ya Kitaifa ya Mazishi. Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Rangwe, Magdaline Chebet, moto huo haukusababishwa na hitilafu ya umeme kwani wakati huo eneo hilo halikuwa na stima. “Tumeondoa uwezekano wa hitilafu ya umeme. Moto huu ulisababishwa na mtu aliyeuwasha kwa makusudi,” alisema Bi Chebet. Uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa petroli ilimwagwa katika baadhi ya sehemu za nyumba kabla ya moto kuwashwa. Wakati wa tukio hilo, hakuna mtu aliyekuwa nyumbani, hali iliyofanya iwe vigumu kwa polisi kupata ushahidi wa moja kwa moja kuhusu chanzo halisi cha moto huo. Kamanda huyo wa polisi alisema alipokea simu usiku kufahamishwa nyumba hiyo ilikuwa ikiteketea. “Tulifika eneo la tukio tukakuta umati mkubwa wa watu waliokusanyika lakini walishindwa kuingia ndani kwa sababu lango lilikuwa limefungwa,” alisema. Nyumba hiyo imezungukwa na ua mkubwa wa mimea, hali iliyoathiri juhudi za uokoaji. Polisi walilazimika kuvunja lango ili kuingia ndani ya uwanja. “Tulipofika, sehemu ya sebule ilikuwa tayari imeteketea. Chumba cha kulala kilikuwa bado hakijaguswa lakini ilikuwa vigumu kukifikia. Vitu vichache tu kutoka jikoni ndivyo viliokolewa,” aliongeza Bi Chebet. Inakadiriwa kuwa mali ya thamani ya mamilioni iliteketea kwenye mkasa huo. Akizungumza baada ya tukio hilo, Dkt Gogo alisema alikuwa Kisumu kwa mipango ya mazishi ya Raila Odinga wakati alipokea simu kuhusu kuchomeka kwa nyumba yake. “Nilikuwa nimelala Kisumu nikishiriki maandalizi ya mazishi ya Mheshimiwa Raila. Sina hakika kilichotokea, nimeshtushwa na kusikitishwa sana,” alisema. Mbunge huyo alitoa wito kwa polisi kufanya uchunguzi wa kina na kuwakamata wote waliohusika na uhalifu huo wa kuchoma nyumba kwa makusudi. Polisi walisema Dkt Gogo alikuwa tayari ameomba ulinzi wa maafisa wa kike wa polisi kabla ya tukio kutokea. Kwa sasa ana mlinzi wa kiume. “Alikuwa ametuma ombi la kuongezewa mlinzi wa kike kutoka ofisini kwangu. Tulikuwa bado tunashughulikia ombi lake moto huo ulipotokea,” alisema Bi Chebet.