MATUMAINI ya miamba wa soka Arsenal kushinda mataji manne msimu huu yaliyeyushwa kwa njia aina yake pale walipofungwa na Manchester City 2-0 kwenye fainali ya Carabao Cup, ugani Wembley. Vinara wa Ligi Kuu ya Uingereza Arsenal walifungwa mabao hayo katika kipindi cha pili wakati nyota wa City O’Reilly alipozidia maarifa safu ya ulinzi dakika ya 60 na 64, kwenye fainali hiyo iliyosakatwa Jumapili, Machi 22, 2026. Vijana wa Mikel Arteta wamekuwa wakifukuzia mataji manne msimu huu wa 2025-26, huku wakiwa kileleni mwa EPL kwa alama 9, wakifuzu kwa robo fainali ya Klabu Bingwa barani Ulaya, wakiwa raundi ya tano ya FA, na vilevile kwenye fainali ya League Cup, almaarufu ‘Carabao Cup’. Katika mechi hiyo ya fainali, The Gunners walianza mchezo kwa mashambulizi makali yakiongozwa na nyota Viktor Gyokeres akishirikiana na kiungo Kai Havertz, ingawa hawakufaulu kuona lango la Man City.