Gen Z waibuka na ‘Niko Kadi’ wanayosema wataitumia kubadilisha uongozi 2027

GEN -Z sasa wamerejea na wito wa ‘Niko Kadi’, kauli-mbiu ambayo wanalenga kuitumia kuwahimiza vijana wajisali kuwa wapigakura nchini kuanzia wiki ijayo ili kubadilisha uongozi wa nchi. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetangaza kuwa kutakuwa na usajili wa wapigakura kuanzia Machi 30. Shughuli hiyo itafanyika kwa siku 30 ikiwalenga wapigakura zaidi ya milioni 2.5. IEBC inakadiria kuwa kutakuwa na wapigakura wapya milioni 6.3 mnamo 2027. Idadi hiyo itaongeza waliojisajili hadi milioni 28.5 katika uchaguzi mkuu ujao. Hata hivyo, kaulimbiu hiyo imeshatekwa na wanasiasa wanaolenga kura za vijana ili kuwika katika uchaguzi mkuu wa 2027. Huku Rais William Ruto akiwataka vijana wajisajili kama wapigakura ili wampigie kura aendeleze uongozi wake, upinzani nao umemkaba koo ukisema vijana wanastahili kujisajili ili kuung’oa uongozi wake mamlakani. Akiongea baada ya kuzindua ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR Kisumu, Rais Ruto alizama kwenye wito wa ‘Niko Kadi’ huku akionyesha kuwa kupitia kura zao, atapata hatamu ya pili. “Kwa washindani wetu, Tuko Kadi. Tuko tayari muda ukifika na tumejiandaa,” akasema Rais Ruto. Hata hivyo, aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua alimshutumu Rais kwa kuteka wito wa vijana kujipigia debe. “Nimewaona mkisema ‘Niko Kadi’, nawaambia Gen-Z wajisajili kama wapigakura kwa sababu ndio njia pekee ya kumtuma Ruto nyumbani.” “Nimeona akiteka nyara wito wa vijana na namwambia kuwa ndiyo una kadi lakini yako ni kadi nyekundu. Unaenda nyumbani,” akasema Bw Gachagua. Aliyekuwa Jaji Mkuu na mwaniaji wa urais wa 2027, David Maraga pia amejiunga na ‘Niko Kadi’ akiwataka wajisajili kwa wingi kama wapigakura. Bw Maraga amesema kuwa iwapo vijana hawatajisajili, Rais Ruto atarejea uongozini mnamo 2027. “Uchaguzi huu ndio utaamua mkondo wa taifa, tafadhali jisajilini na mpige kura. Janga kuu zaidi litakalotikisa Kenya ni Rais Ruto kurejea mamlakani,” akasema. Naibu Kiongozi wa ODM, Godfrey Osotsi na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino pia wamejiunga na ‘Niko Kadi’. Wanasiasa hao wawili ambao ni wanachama wa Linda Mwananchi wamejiunga na wanaowataka vijana wapige kura. “Ninaunga wito wa Niko Kadi ili vijana wajisajili na waamue mkondo au mwelekeo wa nchi yao,” akasema Bw Osotsi. Seneta wa Kitui, Enoch Wambua pia amewataka vijana watumie wito huo kupata vitambulisho na kujisajili kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu ujao. “Huu ndio wakati wa kujibu uongozi mbaya wa Rais Ruto kwa sababu sauti yao ndiyo itaamua matokeo ya uchaguzi mkuu ujao,” akasema Bw Wambua ambaye ni mwandani wa kisiasa wa Kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka. Gen-Z katika chaguzi zilizopita wamekashifiwa kwa kupenda tu masuala ya mitandaoni badala ya kupiga kura kwenye uchagujzi mkuu. Takwimu zinaonyesha idadi yao waliojitokeza kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 ilikuwa chini. Hata hivyo, waligutuka kupitia Mswada wa Fedha wa 2024 ambao ulikuwa na mapendekezo mengi ya kuongeza ushuru. Waliandaa maandamano makubwa yaliyosababisha Rais Ruto atupilie mbali mswada huo na kuvunja Baraza lake la Mawaziri. Kwa mujibu wa Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS), idadi ya vijana nchini (walio chini ya umri wa miaka 35) ni asilimia 75 ya milioni 47.6 ya Wakenya. Vijana waliozaliwa miaka ya 1,990 na 2010 wamekataa kujihusisha na mrengo wowote wa kisiasa wakisema hawana ukabila. Kwa mujibu wa Prof David Mondo, mchanganuzi wa masuala ya kisiasa na mhadhiri, Rais Ruto analenga kutumia kadi kuwachanganya vijana na kusababisha wengi wao wasijitokeze kujisajili kura. Prof Mondo anasema vuguvugu la ‘Niko Kadi’ linalenga kusababisha Rais Ruto ahudumu kwa muhula mmoja kutokana na mauaji ya Gen-Z katika maandamano ya 2024 na utawala mbaya. “Upinzani nao unalenga kutumia Niko Kadi kuongeza kura zao. Vuguvugu hili hata hivyo ni mwiba kwa serikali na pia kuwaadhibu Gen-Z ambao walipigia Mswada wa 2024 kura,” akasema Prof Monda. Anaongeza kuwa tatizo kwa Gen Z litakuwa ni kulinda kura zao, kuzuia wizi wa kura na kuhakikisha Niko Kadi inasalia hadi 2027 na hata baada ya uchaguzi mkuu.