LA TAIFA LEO
CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kimegawanyika wazi huku mikutano miwili iliyofanyika kwa wakati mmoja jijini Nairobi ikidhihirisha vita vya uongozi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Katika mkutano wa wajumbe maalum uliofanyika Jamhuri Grounds mnamo jana, Seneta wa Siaya Oburu Oginga aliidhinishwa rasmi kuwa kiongozi wa chama, hatua iliyochukuliwa kama mabadiliko makubwa ndani ya ODM. Hatua hiyo ilipuuzwa na mrengo wa pili wa Linda Mwananchi unaohusisha viongozi vijana ulioandaa mkutano wa pili katika Ufungamano House chini ya Katibu Mkuu Edwin Sifuna. Uamuzi wa kuidhinisha Dkt Oburu ulipitishwa kwa kauli moja na wajumbe, huku Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed akitangaza matokeo baada ya hoja kuwasilishwa na kuungwa mkono. Pamoja na kuthibitishwa kwa Oburu, wajumbe walimpa mamlaka ya kuanzisha mazungumzo ya kisiasa na chama cha United Democratic Alliance kinachoongozwa na Rais William Ruto kabla ya 2027. Katika mkutano huo pia, Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir na mwenzake wa Kisii Simba Arati waliidhinishwa kuwa manaibu viongozi wa chama, huku Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi akiondolewa katika safu ya uongozi katika kile kilichoelezwa na baadhi ya wachambuzi kama “kusafisha” viongozi wanaoonekana kupinga mwelekeo mpya. Mwenyekiti wa chama, Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, alisisitiza kuwa mkutano huo ndio pekee uliokuwa halali kikatiba, akisema uliitishwa kwa kufuata taratibu zote za chama. Katika mkutano huo huo, Winnie Odinga alijitokeza na kutoa hotuba iliyotikisa siasa za ODM. Binti huyo wa Raila Odinga, ambaye hapo awali alionekana kuunga mkono mrengo wa Edwin Sifuna, alibadili msimamo na kuunga mkono mjomba wake Oburu. “Siku chache zilizopita nilisema ODM ni nyumbani, ninasimama hapa kama sauti ya vijana wenye matumaini,” alisema. Alionya kuwa chama kinaweza kupoteza mwelekeo iwapo hakitazingatia wananchi wa kawaida. “Tunapaswa kurejea maadili yaliyotujenga miaka 20 iliyopita,” aliongeza. Winnie alitoa wito wa kuanzishwa kwa “ODM mpya” inayolenga kuvutia vijana, kuhimiza mazungumzo na maridhiano, pamoja na kupigania haki za kijamii na waliodhulumiwa. “ODM ni nyumbani, lazima turudi kwa maadili yaliyounda chama hiki miaka 20 iliyopita,” alisema huku akionya kuwa chama kina hatari ya kujitenga na wananchi wa kawaida. Hata hivyo, wakati mkutano huo ulipokuwa ukiendelea Jamhuri Grounds, mrengo wa Sifuna pamoja na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na Gavana wa Siaya James Orengo chini ya vuguvugu la “Linda Mwananchi” uliupuuza. Sifuna alisema mkutano wa Dkt Oburu na mrengo wake haukuwa halali na unalenga kuua misingi ya chama. “Chama chetu kiko hatarini, watu wenye nia mbaya wamepenya ndani yake. Hatutakubali maadili ya Raila Odinga yapotoshwe,” alisema. Aidha, alikataa wazi kufanya kazi chini ya uongozi wa Oburu, akisema hawezi kuwa Katibu Mkuu wa kiongozi anayelenga kuunga mkono utawala unaopuuza Wakenya. Kauli hiyo ilionyesha wazi ufa mkubwa ndani ya chama ambao itakuwa vigumu kuuziba. Bw Osotsi, Orengo na Owino walitetea Linda Mwananchi wakisema linalenga kulinda haki za wananchi na kushinikiza fidia kwa familia za waliouawa, huku pia likipigania ajira kwa vijana. “Sisi tunalinda wananchi na haki zao,” alisema Bw Owino akitaja mrengo wao kama ODM halali inayoshikilia maadili na Raila Odinga. Mkutano huo uliendelea hata polisi waliporipotiwa kujaribu kuuvuruga, hali iliyoongeza joto la kisiasa ndani ya chama hicho.. Katika hotuba yake ya kwanza baada ya kuidhinishwa, Oburu alitoa onyo kali dhidi ya utovu wa nidhamu, migawanyiko na uasi wa ndani ya chama. “Demokrasia si fujo wala chuki, bali ni kufuata misingi yake,” alisema kwa sauti tulivu lakini thabiti. Alisisitiza kuwa ODM inalenga mamlaka na haitayumba. “Hatuoni aibu kusema tunataka mamlaka, na tutabaki na mamlaka. Bila mamlaka huwezi kutekeleza sera yoyote,” alisema huku wajumbe wakishangilia. Ingawa alikataa kufanya kazi na Oburu Sifuna alisema hayuko tayari kuondoka katika chama hicho, akisisitiza kuwa yuko tayari kukabiliana na wapinzani wake kupitia uchaguzi huru na wa haki badala ya kile alichokitaja kuwa mbinu zisizo halali za kumng’oa. Badala ya kurudi nyuma, Sifuna aligeuza mzozo huo kuwa vita vya mchakato na mamlaka, akiwataka wanaotaka kumuondoa kuitisha mkutano mkuu halali wa Wajumbe wa Kitaifa (NDC), ambao ndio chombo cha juu zaidi cha maamuzi katika chama hicho. “Chama chetu kiko hatarini. Tunataka twende kwa NDC ambapo kila mwanachama atapiga kura. Nafasi zote za uongozi hutolewa na wanachama. Hakuna mtu anaweza kukaa na kufikiria kuwa Sifuna ataondolewa kwa njia hii,” alisema. Alisema imekuwa heshima kubwa kwake kuhudumu kama Katibu Mkuu chini ya marehemu Raila Odinga, akipuuza wito wa kujiuzulu. “Nilihudumu kama Katibu Mkuu kwa miaka minane, halafu leo mnaniambia niwe katibu mkuu wa kutumiwa? Namwambia Oburu tafuta Katibu Mkuu wako, mimi siwezi kuwa wako,” alisema huku akishangiliwa. Bw Orengo alitoa wito kwa Wakenya kuendelea kupigania haki zao, akihusisha mapambano ya sasa na yale ya uhuru. “Uhuru hupatikana kupitia mapambano. Vijana lazima wasimame kutetea haki zao,” alisema, akitangaza maandamano ya Juni 24 kuwakumbuka vijana waliouawa katika maandamano ya hivi majuzi.
Go to News Site