Collector
NCIC: Huenda kukatokea ghasia kabla na baada ya uchaguzi 2027 | Collector
NCIC: Huenda kukatokea ghasia kabla na baada ya uchaguzi 2027
LA TAIFA LEO

NCIC: Huenda kukatokea ghasia kabla na baada ya uchaguzi 2027

TUME ya Kitaifa ya Uwiano na Utengamano (NCIC) imeonya kuhusu kuongezeka kwa mvutano wa kisiasa, matamshi ya chuki na migogoro ya kijamii huku nchi ikijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2027. Tume hiyo iliyoanzishwa baada ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 kwa lengo la kukuza umoja wa kitaifa na kuzuia ghasia za kikabila, imeambia wabunge kuwa ushindani wa kisiasa unatarajiwa kuwa mkali katika kipindi kijacho cha uchaguzi. Katika mawasilisho yake kwa Kamati ya Bunge kuhusu Utawala na Usalama wa Ndani kuhusu bajeti ya mwaka wa 2026/2027, NCIC ilisema imepewa Sh711 milioni pekee katika makadirio ya bajeti ilhali inahitaji Sh1.5 bilioni. Afisa Mkuu Mtendaji wa NCIC, Daniel Mutegi, alisema fedha hizo hazitoshi kufadhili shughuli za mapema za kufuatilia maeneo yenye migogoro na kuzuia matamshi ya chuki kabla hali haijawa mbaya. “Tunahitaji fedha nyingi kwa ajili ya mifumo ya tahadhari ya mapema, kutambua maeneo yenye migogoro na kuandaa mazungumzo ya kudumisha amani katika jamii mbalimbali,” alisema Dkt Mutegi mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Gabriel Tongoyo. Alisema sehemu kubwa ya matamshi ya chuki sasa yanaenezwa kupitia mitandao ya kijamii, jambo linalohitaji vifaa vya kisasa vya kiteknolojia ili kufuatilia wahusika na kukusanya ushahidi wa kutosha kuwasilishwa mahakamani. “Bila vifaa bora vya kisasa, huenda tukashindwa kudhibiti uhalifu wa matamshi ya chuki mitandaoni,” alisema. Kulingana na Kifungu cha 96 cha Sheria ya Adhabu, mtu anayepatikana na hatia ya kueneza matamshi ya chuki anaweza kufungwa hadi miaka mitano gerezani. Hata hivyo, NCIC ilikiri kuwa changamoto ya kukubalika kwa ushahidi wa kiteknolojia mahakamani imekuwa ikiwapa wakati mgumu waendesha mashtaka. Baadhi ya wabunge walikosoa tume hiyo wakisema imekuwa ikidai fedha zaidi kila mwaka bila kuonyesha matokeo ya kuridhisha katika kukabiliana na matamshi ya uchochezi. Naibu mwenyekiti wa kamati hiyo, Dido Raso, aliiaumu NCIC kwa kushindwa kuchukua hatua kali dhidi ya viongozi wa kisiasa na watu wanaowatukana viongozi wa taifa mtandaoni. “Tunakaribia uchaguzi mkuu na ikiwa NCIC haitabadilika, kamati hii inaweza kukataa kuiongezea fedha kwa sababu wananchi hawaoni kazi yake,” alisema Bw Raso. Mbunge wa Sotik, Francis Sigei, pia alihoji umuhimu wa tume hiyo akisema Wakenya wanahitaji kuona hatua za vitendo badala ya maelezo mengi. Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Raymond Omollo, alitetea NCIC akisema changamoto zake zimechangiwa na ukosefu wa makamishna wa kutosha. Tume hiyo pia ina hofu ya kurejea kwa ghasia kama za baada ya uchaguzi wa 2007/2008 zilizoua zaidi ya watu 1,300 huku maelfu wakifurushwa makwao. NCIC imesema itaendelea kuhimiza amani, uvumilivu na mshikamano wa kitaifa ili kuzuia Wakenya kupigana kabla na baada ya uchaguzi wa 2027

Go to News Site