LA TAIFA LEO
UAMUZI wa jana kuhusu kesi ya kuondolewa mamlakani kwa aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua una athari kubwa za kisiasa kwa kiongozi huyo wa chama cha DCP pamoja na wanasiasa wengine muhimu, akiwemo Rais William Ruto, kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Wakati tukielekea mtamboni jana usiku, maamuzi mengi kuhusu utetezi wa Bw Gachagua yalikuwa yameenda kinyume na matarajio yake, hali iliyomaanisha atalazimika kuelekea katika Mahakama ya Rufaa kutafuta afueni. Mahakama Kuu jana, kupitia jopo la majaji watatu Anthony Mrima, Eric Ogolla na Freda Mugambi, iliamua kuhusu malalamiko yaliyoibuka baada ya Gachagua kufukuzwa madarakani. Kwa mujibu wa sehemu ya hukumu iliyosomwa na Jaji Ogola, Mahakama ilisema madai ya upendeleo, mgongano wa maslahi na uamuzi wa awali dhidi ya Spika wa Bunge la Kitaifa, Spika wa Seneti, wabunge na maseneta hayakuungwa mkono na ushahidi wa kutosha na wa moja kwa moja. Katika uamuzi wake, mahakama ilisema kuwa mchakato wa kushirikisha umma katika harakati ya kumtimua Bw Gachagua ulifikia kiwango cha kuridhisha kinachohitajika kikatiba, licha ya kuwepo kwa changamoto chache za kiutendaji katika baadhi ya maeneo. Majaji walibainisha kuwa Katiba haihitaji ushiriki wa umma uwe mkamilifu bila dosari yoyote, bali inataka wananchi wapewe fursa ya kweli na yenye maana ya kutoa maoni yao kuhusu masuala yanayowahusu. Kwa msingi huo, jopo hilo lilikataa madai ya walalamishi waliodai kuwa ushiriki wa umma ulikuwa hadaa na haukukidhi matakwa ya kikatiba. Uamuzi huo ni miongoni mwa hoja muhimu zilizokuwa zikisubiriwa katika kesi ya kupinga kuondolewa kwa Gachagua mamlakani, huku ukiimarisha msingi wa hatua zilizochukuliwa na Bunge la Kitaifa kuelekea kumng’atua kwa Bw Gachagua. Kuhusu suala la upendeleo katika kesi ya kuondolewa madarakani kwa Gachagua, majaji walifikia hitimisho kwamba madai hayo hayakuthibitishwa. Uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu kesi nzima ya kutimuliwa madarakani kwa Bw Gachagua, unachukuliwa kuwa mojaespo ya maamuzi muhimu zaidi ya kisiasa na kisheria nchini Kenya katika miongo michache ya hivi karibuni. Matokeo ya kesi hii hayataathiri tu mustakabali wa kiongozi huyo, bali pia huenda yakabadili muundo wa siasa za taifa. Moja ya masuala makuu ni mustakabali wa kisiasa wa Gachagua mwenyewe. Kifungu cha Sita cha Katiba ya Kenya kinasema wazi kwamba afisa wa umma aliyeondolewa mamlakani hawezi tena kushikilia nafasi yoyote ya umma kwa miaka 10. Hii ina maana kwamba Gachagua hatashiriki katika uchaguzi wa urais au kiti kingine mwaka 2027. Hata hivyo, Gachagua anaweza kutumia mwanya wa kisheria kuwania kwenye uchaguzi wa 2027. Ikiwa atakata rufaa kabla ya uchaguzi, wanasheria wake wanaweza kudai haki yake ya kikatiba ya kuwania chini ya Kifungu cha 38 hadi pale Mahakama itakapoamua rufaa yake. Yeye mwenyewe amesema kabla ya rufaa kuamuliwa, angali na nafasi ya kugombea urais katika uchaguzi ujao. “Iwapo Gachagua ataruhusiwa kuwania urais, hii inaweza kubadilisha hali ya kisiasa nchini. Wagombea wa upinzani wanaweza kugawana kura zao, jambo litakalorahisisha ushindi wa Rais Ruto. “Hii ni hali ambayo inaweza kuunda tena mwelekeo wa siasa za 2027,” asema mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki. Kulingana na Dkt Gichuki, uamuzi huo ni mwanzo wa mchakato wa kisheria unaoelekea Mahakama ya Rufaa, huku taifa likiangalia kwa makini hatua ambayo Gachagua na washtakiwa watachukua. “Kila upande unaweza kukata rufaa. Gachagua, walalamishi wengine na washtakiwa ikiwemo Bunge la Kitaifa na Seneti,” asema. Uamuzi huu hautaathiri tu Gachagua na Rais Ruto, bali pia unatazamiwa kuathiri matarajio ya kisiasa ya viongozi wengine wakuu, ikiwemo Kalonzo Musyoka wa Wiper na Dkt Fred Matiang’i wa Jubilee, huku taifa likijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2027. Wawili hao wanatarajia kuungwa mkono na Gachagua kwa tiketi ya urais kupitia muungano wa upinzani. “Matokeo haya ya kesi yanatarajiwa kuunda mwelekeo mpya wa kisiasa na kupatia nguvu upinzani au kuufanya ugawanyike. Ni kigezo cha kupima mshikamano wa upinzani,” asema Dkt Gichuki. Mbali na Rais Ruto na Bw Gachagua, matokeo ya kesi hiyo yanaweza pia kuathiri matarajio ya kisiasa ya kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na naibu kiongozi wa chama cha Jubilee, Fred Matiang’i, ambao wote wanatajwa kama wagombeaji wanaoweza kuwania urais kupitia muungano wa upinzani.
Go to News Site