LA TAIFA LEO
JAJI Mkuu Mstaafu David Maraga Jumatatu alikuwa kati ya watu walionyakwa wakati wa maandamano ya amani ya kupinga mpango wa serikali kuanzisha kituo cha kuwatunza wanyama katika mbuga ya Nairobi. Serikali inapanga kuanzisha mradi huo kwenye sehemu ya ardhi ambayo ipo ndani ya msitu huo. Bw Maraga alijiunga na mamia ya wanaharakati katika kupinga mradi huo. Alisema kuwa kama mwaniaji wa urais wa UGM, hawezi kukimya na kuona msitu ndani ya mbuga hiyo ukifyekwa katika hali tatanishi. Licha ya maandamano hayo kuidhinishwa na kamanda wa kieneo wa polisi, ambao walikuwepo kuhakikisha sheria inafuatwa, waandamanaji walinyakwa na polisi ambao walikuwa wamevalia kiraia. Waandamanaji hao walikuwa wamepanga kuwasilisha malalamishi yao kwa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS). Hata hivyo, hawakufaulu kwa kuwa walikabiliwa na polisi wa kupambana na ghasia. “Hajashtakiwa lakini tunasubiri mwelekeo kutoka kwa polisi ambao wamewakataza mawakili wake kuangalia maelezo yaliyonakiliwa kwenye OB. Bado tunasubiri,” akasema Mwenyekiti wa UGM Agostinho Neto. Kwenye mahojiano na Taifa Leo akisubiri kuachiliwa, Bw Maraga alidai kuwa polisi katika kituo hicho walikuwa wakifuata ‘amri’ kutoka juu. Alidai kuwa watu wenye ushawishi walikuwa wakizuia kuachiliwa kwake. “Kile ambacho tunafahamu ni kuwa amri ilitoka juu na hata Mkuu msimamizi wa kituo (OCS) akija, bado hatutaachiliwa,” akasema Bw Maraga.
Go to News Site