LA TAIFA LEO
MAHAKAMA kuu Jumatatu jioni ilikataa kuharamisha kutimuliwa kazini kwa aliyekuwa naibu Rais Rigathi Gachagua lakini ikaamuru alipwe fidia ya Sh50 milioni. Majaji Eric Ogolla, Antony Mrima na Freda Mugambi waliagiza serikali imlipe fidia hiyo wakisema Bunge la Seneti lilijadili kuondolewa mamlakani kwa Gachagua akiwa mgonjwa. Majaji hao walisema haki za Gachagua zilikandamizwa wakati Seneti ilikataa kuahirisha mjadala wa kumtimua kazini alipougua na kulazwa Karen Hospital. “Bunge la Seneti liliendelea kujadili kutimuliwa kwa Gachagua licha ya kuelezwa alikuwa mgonjwa na alikuwa amelazwa Karen Hospital,” majaji hao walisema katika uamuzi uliosomwa kwa masaa 10. Katika uamuzi huo wa kihistoria, majaji hao walisema licha ya kasoro za Bunge la Seneti, uamuzi wa kumuondoa kazini utasimama. “Makosa ya Seneti hayaharamishi uamuzi wa bunge la kitaifa wa kumtimua kazini Gachagua,” majaji hao walisema. Bunge la kitaifa lilimpata Gachagua na hatia ya kuchochea ukabila, kutumia vibaya mamlaka ya afisi yake. Alikabiliwa na mashtaka 11. Hoja ya kumtimua kazini Gachagua iliwasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse. Majaji hao walisema kwamba hawataamuru Bw Gachagua arudishwe kazini wakisema “itasababisha mtafaruku wa kikatiba kwa vile Prof Kithure Kindiki aliteuliwa na anaendelea kuhudumu.” "Katiba kamwe hairuhusu manaibu wawili wa rais kuhudumu kwa wakati mmoja,”majaji hao watatu walisema. Uamuzi huo ulitamatisha mojawapo ya kesi zilizosababisha mkwaruzano wa kisheria na ustawishaji wa mustakabali wa sheria nchini. Baada ya Seneti kuidhinisha kutimuliwa afisini kwa Gachagua Oktoba 2024 na kuteuliwa kwa Prof Kindiki kutwaa wadhifa huo, kesi 41 ziliwasilishwa kortini kupinga uamuzi huo wa kumwondoa mamlakani. Katika kesi hiyo Gachagua na walalamishi wengine 40 walikosoa mabunge mawili wakidai maoni ya wananchi hayakusakwa kwa mujibu wa sheria. Majaji hao walitupilia mbali baadhi ya madai ya Bw Gachagua huku wakisema mahakama kuu iko na uwezo wa kuhoji uamuzi wa Seneti "Hakuna asasi ya serikali ikiwa ni pamoja na bunge, ambayo haiwezi kuhojiwa na mahakama kuu haswa inapodaiwa ilikandamiza Katiba," majaji hao walisema. Majaji hao walitupilia mbali mawasilisho ya Bunge na Mwanasheria Mkuu kwamba kutimuliwa kazini kwa Bw Gachagua lilikuwa suala la kisiasa na halimo chini ya usimamizi wa mahakama kuu. Walisema haki za Gachagua kwa mujibu wa Vifungu 47 na 50 vya Katiba haviwezi kuzuia kutimuliwa kwake kwa mujibu wa kifungu 145 cha Katiba. "Ni barabara kwa Gachagua kukoma kuwa naibu rais kwa mujibu ya kifungu 145 cha katiba,” mahakama ilisema. Hata hivyo, majaji hao walisema haki ya Gachagua kufuatia kukandamizwa na kukiukwa kwa haki zake kwa kutopewa muda wa kujitetea kunaweza gharamiwa tu kwa kulipwa fidia. Uamuzi huo ulizua hisia kali huku wakili mwenye tajriba ya juu (SC) Paul Muite aliyemwakilisha Gachagua akisema atakata rufaa. Lakini wakili Prof Tom Ojienda aliyewakilisha Seneti alipongeza uamuzi huo akisema “Gachagua alitimuliwa kazini kwa mujibu wa sheria.” Bw Gachagu hakuhudhuria kusomwa kwa uamuzi wa kesi hiyo.
Go to News Site