LA TAIFA LEO
SPIKA wa Bunge la Kitafa Moses Wetang’ula huenda akabururwa kortini baada ya kundi la wabunge wa upinzani kuanzisha mchakato wa kumfungulia mashtaka kwa kukaidi amri ya korti kuhusu uamuzi wa kumpiga marufuku Mbunge wa Kitutu Chache Kusini, Anthony Kibagendi kuingia bungeni. Wabunge hao wanaoegemea Linda Mwananchi, kundi lisilo rasmi la wabunge wa ODM wakiongozwa na Maseneta Edwin Sifuna (Nairobi) na Godfrey Osotsi (Vihiga), na wabunge Caroli Omondi (Suba Kusini) na Babu Owino (Embakasi Mashariki) waliapa kumfanya Spika Wetang’ula kuwajibika binafsi. Wabunge hao waliojumuisha vilevile Seneta, Dan Maanzo (Makueni) na wabunge Joshua Kimilu (Kaiti) na Obadia Barongo (Bomachoge Borabu), walihoji kuwa Spika Wetang’ula kukataa kumrejesha Kibagendi ni shambulizi la moja kwa moja dhidi ya utawala wa sheria na jaribio la kugeuza Bunge la Kitaifa kuwa kinga ya serikali inayoegemea upande mmoja. “Uamuzi huo wa Spika ni haramu, kinyume cha katiba na tutashinikiza kupitia korti mashtaka ya kudharau agizo la mahakama yafunguliwe dhidi yake kwa kukaidi amri ya korti,” alisema Seneta Sifuna. Kulingana na Seneta Sifuna, “tatizo pekee la Kibagendi ni kwamba amefuatilia masuala ya ufisadi katika Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) na wanataka kuua sauti yake bungeni kwa sababu wanajua hapo ndipo watu walitutuma kuwawakilisha.” “Kama tunauliza maswali kuhusu ufisadi kwenye SHA, iwapo inafanya kazi au la, hilo ni jukumu letu kama wawakilishi wa watu. Kwa mtu yeyote kujaribu kuwadhulumu wabunge kwa kufanya kazi yao tni jambo linalohitaji kukemewa.” Bw Kibagendi, ambaye amekuwa akizungumzia sana kuhusu usimamizi mbaya na ubadhirifu wa fedha za umma katika SHA, alisaka afueni katika Mahakama Kuu. Februari 17, Spika Wetang’ula pasipo kumba haki ya kimsingi ya kusikizwa baada ya kuzua maswali kuhusu uhuru wa bunge kwa kusema imekuwa “jumba la mnada” katika mahojiano ya televisheni yaliyopeperushwa moja kwa moja, alimfurusha Kibagendi kwa muda usiojulikana hadi atakapoomba radhi kwa “Bunge” kupitia karani. “Sitamwalika mbunge afafanue kwa sababu niliona na macho yangu mwenyewe na kusikia kwa masikio yangu,” alisema Spika Wetang’ula. “Utafungiwa nje ya vikao vya Bunge hili hadi utakapoleta ombi lililonakiliwa vyema la msamaha. Hutaleta kwangu, kwa sababu nimezoea kutukanwa, lakini kwa Bunge kwa kuidhihaki,” alisema Spika. Bw Kibagendi alifika kortini ambapo Mahakama Kuu, Machi 19, 2026, ilisitisha kwa muda uamuzi wa Spika kumzuia kufika bungeni na kumrejeshea kikamilifu majukumu yake kama mwakilishi wa watu akisubiri uamuzi wa kesi yake. Hata hivyo, Kibagendi alipofika Bungeni Machi 31, akiwa amejihami kwa amri ya korti kumkabidhi Spika na Bunge, alizuiwa na Mbunge wa Homabay, Peter Kaluma, aliyekuwa spika wa muda wakati huo.
Go to News Site