Collector
Kauli mpya ya Trump yazima matumaini ya kusitishwa kwa vita dhidi ya Iran | Collector
Kauli mpya ya Trump yazima matumaini ya kusitishwa kwa vita dhidi ya Iran
LA TAIFA LEO

Kauli mpya ya Trump yazima matumaini ya kusitishwa kwa vita dhidi ya Iran

WASHINGTON, Amerika MATUMAINI ya kumalizika kwa vita kati ya Amerika-Israel na Iran yameyeyuka baada ya Rais Donald Trump kuahidi kwamba bado wataendeleza mashambulizi dhidi ya Iran. Hii ni licha ya kuwa tayari kuna kilio vita hivyo vimechangia uhaba wa mafuta na kupandisha bei ya bidhaa hiyo baada ya Iran kufunga Strait of Hormuz. “Tutaendelea kuwapiga kwa zaidi ya wiki mbili au tatu zinazokuja na tuwarejesha enzi za zamani ambako wanastahili kuwa,” akasema Trump mnamo Jumatano akihutubu Amerika. Hasa Trump alisema watakuwa wakiyalenga viwanda vya kawi vya Iran pamoja na miundomsingi yao ya mafuta. Kwa Trump, lazima viongozi wa Iran wakubali kuwa wameshindwa vitani na pia waridhie matakwa yote ya Amerika. Wanajeshi wa Iran nao wamemjibu Trump, Amerika na Israel wakisema wapo tayari kukabiliana nao na kuendeleza mashambulizi. Ebrahim Zolfaqari, Msemaji wa jeshi la Iran alisema wapo tayari vita hivyo viendelee ‘milele’ hadi Amerika na Israel zijute na maadui wa Tehran wajisalimishe. Vita hivyo vimesababisha uhaba wa mafuta ambao umeanza kuathiri bara Asia na unatarajiwa kutikisa Ulaya hivi karibuni. Tayari Italia imeonyesha hofu yake kuwa wataathirika pakubwa kutokana na uhaba wa mafuta vita hivyo vikizidi kuendelea. Maelfu ya watu wameuawa Mashariki ya Kati tangu Februari 28 wakati ambapo Amerika-Israel zilishambulia Iran. Nayo Tehran ilijibu kwa kushambulia Israel pamoja kambi za jeshi za Amerika mashariki ya kati na ukanda wa Gulf. Alhamisi, Israel ambayo imekuwa ikipambana kuangusha droni za Iran ilithibitisha kuwa bado inashambuliwa huku Saudi Arabia na Abu Dhabi zikisema ziliangusha droni zilizokuwa zimetumwa kutoka Iran. Amerika pia imetoa tahadhari na kuamrisha raia wake kwenye ubalozi wake Baghdad waondoke Iraq. Hii ni kutokana na hofu ya kushambuliwa na wapiganaji wanaoegemea upande wa Iran.

Go to News Site