LA TAIFA LEO
TULIPOMTEMBELA Judith Munyasa katika kijiji cha Nzoia A, Kaunti ya Bungoma, tulimpata akikagua viazi alivyovuna siku chache zilizopita. Pamoja na wanawe, Judith, aliyejaaliwa watoto watano, anapanga viazi hivyo akiangalia vya kuwauzia wateja na vile anavyotarajia kuhifadhi kama mbegu atakazopanda msimu ujao. “Nilinunua mbegu ambazo ubora wao umehitimu kiwango kinachofaa na nimerudia kuzipanda na bado nitarudia kuzipanda tena kwa mara ya mwisho kabla ya kununua tena mbegu zingine. Pia huwa nikipanda, sirudii sehemu ambapo nilipanda viazi awali, ila nazipanda katika sehemu tofauti ya shamba. Hii inasaidia kuzuia magonjwa na pia kuhakikisha napata mavuno bora na mengi,” anaeleza Akilimali. Kando na viazi, Judith, pia ni mkulima wa mahindi na maharagwe kwenye shamba lake la ekari mbili. Mkulima huyu ambaye amebobea katika kilimo kinacholenga kuhifadhi mazingira, anasema mbinu hii alianza mwaka wa 2022 baada ya kupokea mafunzo kuhusu kilimo, hali anayosema ina manufaa kadhaa kwake. “Kilimo kinachohifadhi mazingira hupunguza mmomonyoko wa udongo, huongeza ubora wa udongo kwenye shamba langu na mavuno pia huongezeka. Faida nyingine ya kilimo hiki ni kuwa si lazima mkulima awe na shamba kubwa ndiyo upate mavuno mengi, kutunza shamba ndiyo kitu cha maana,” anaongeza. Anasema mfumo huo wa kilimo huhakikisha kuwa hautatizi udongo wakati wa kuandaa shamba. Utaratibu huo, anaeleza humrahisishia kazi wakati wa kupalilia ambapo hutumia trekta. “Hii trekta niliichukua kwa mkopo, sijamaliza kuilipia, kwa sababu nailipa pole pole kila wiki kulingana na jinsi naitumia kufanya kazi. Imekuwa na manufaa hadi kwa wakulima wenzangu ambao huwa nawapalilia mashamba yao kwa kutumia hii trekta.” Hatua yake ya kununua trekta anasema imesaidia kuimarisha kilimo chake, na kwamba hali ni tofauti sana na alipoanza kilimo miaka iliyopita. Hata hivyo, juhudi zake zilipigwa jeki na uamuzi wake wa kujiunga na Chama cha Wakuzaji Nafaka (Cereal Growers Association) mwaka wa 2021 na kupata mafunzo ya kilimo biashara. “Kuanzia mwaka wa 2022 nilipoanza kuhudhuria warsha za mafunzo kwa wakulima, nilifundishwa na wakulima wengine jinsi ya kufanya kilimo biashara ili kupata pesa za kugharamia mahitaji mengine kama kulipia watoto karo na shughuli zingine,” anasema. Kutokana na mafunzo hayo, ndiyo alianza kuzingatia kilimo cha kuhifadhi mazingira kwenye shamba lake. “Sasa hayo mafunzo yalianza kunisaidia kwa kubadilisha kilimo changu. Pia nilianza kutumia mbolea ambazo hazina madhara kwenye udongo wakati wa upanzi jinsi tulivyofundishwa. Na kweli nilipoanza kutumia hizi mbolea, niliona mavuno yangu yalianza kubadilika.” Punde matunda ya mafunzo hayo yalianza kuonekana na majirani wake walianza kutafuta maarifa kutoka kwake. Kadri mkulima mmoja baada ya mwengine alipofika katika boma lake, kutaka mafunzo hayo ndipo alihisi umuhimu wa kuwahamasisha. Miaka minne baadaye, Judith, sasa ana idadi kubwa ya wakulima wanaopata mafunzo kutoka kwake. Wakulima hao wanafanya kilimo katika kaunti za Bungoma, Kakamega na Vihiga. Yeye huuza mazao yake katika soko la karibu na pia kupitia mitandao yake maarufu, Juddy farmers service centre. Hata hiyo, anasema kungali na changomoto ya kuuzia wateja mmoja mmoja kwani kila mtu hununua kulingana na bei anayohisi ni sawa. “Kama mkulima changomoto ni kupata bidhaa za shamba kwa bei tofauti. Kwa mfano, bei inapanda juu wakati wa kupanda alafu wakati unavuna kama mkulima unauza bidhaa zako kwa bei ya chini. Ukipata mnunuzi ambaye amekuja anataka mahindi mengi kwa wakulima, ile bei anayosema inakuwa ya kuvunja mioyo,” anaeleza. Pia anataja changamoto zinazosabbabishwa na mabadiliko ya hali ya anga. “Wakati mwingine unapanda vizuri lakini mvua inanyesha ya mawe unapata hasara hata kabla ya kuvuna. Msimu uliopita pia kulikuwa na changamoto ya kiangazi nikapata mavuno machache.”
Go to News Site