LA TAIFA LEO
LICHA ya chama tawala UDA na kile cha ODM kuungana katika Serikali Jumuishi, migawanyiko ya viongozi kutoka eneo la Pwani inaendelea kujitokeza huku wafuasi wa vyama hivyo wakionyeshana ubabe wa kisasa. Kikosi cha UDA kinachoongozwa na Waziri wa Michezo Salim Mvurya pamoja na Katibu Mkuu wa chama Hassan Omar kinazidi kuimarika. Hii ni baada ya vyama vya Pamoja African Alliance (PAA) chake Spika wa Seneti Amason Kingi na kile cha Amani National Coalition (ANC) kutangaza kuwa havitasimamisha wagombeaji katika uchaguzi mkuu wa 2027, na badala yake vitaunga mkono wawaniaji wa UDA. Kwa upande mwingine, Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini Hassan Joho pamoja na Naibu Kinara wa ODM ambaye pia ni gavana wa Mombasa, Abdulswamad Nassir, wamekuwa mstari wa mbele kupigia debe chama cha chungwa. Wameeleza kuwa wanaunga mkono Rais William Ruto katika azama yake ya kuwania awamu ya pili, lakini viti vingine vyote pamoja na kile cha Naibu Rais viko wazi kuwaniwa na mwanachama yeyote wa ODM. Wiki hii kikosi cha UDA kilipaga kambi katika Kaunti ya Tana River ambapo kilianzisha hamasisho kwa wakazi kujiandikisha kupiga kura na pia kuwa wanachama wa UDA, huku kikimpigia debe Rais Ruto. “Tutaendeleza mpango huu wa kuhamasisha wakazi wa Pwani kujisajili kwa wingi ili kuhakikisha William Ruto anapata ushindi mkubwa wa muhula wa pili. Pia wakati huu tunataka kupata wafuasi na viti vingi eneo la Pwani,” alisema Omar. UDA tayari imeweka vigogo katika ngome zilizomilikiwa na ODM kama vile Kilifi, Mombasa na Tana River jambo ambalo halijafurahisha wanachungwa. Huko Kilifi aliyekuwa Waziri wa Jinsia Aisha Jumwa amejitosa uwanjani kumpinga Gavana wa sasa wa ODM, Gideon Mung'aro.Naye Omar ananoa makali kukabiliana na Gavana Nassir kule Mombasa. Hussein Dhado wa UDA anajipanga kumrithi Gavana wa Tana River, Dhadho Godhana, ambaye anamaliza muhula wake wa pili. Hata hivyo, mbinu za UDA kujaribu kutwaa uongozi kutoka kwa chama cha ODM zinaonekana kukinzana na mipango ya ODM, ambayo imeapa kupambana kufa kupona kuhakikisha chama hicho kimesalia imara. “Licha ya kinara wa chama cha ODM Raila Odinga kuondoka, tutaendeleza sera zake. Wapinzani wajue chama bado kiko imara na tutachukua viti vingi katika uchaguzi mkuu ujao. Kiti ambacho hatutagombea ni cha uraisi,” akahoji Gavana Nassir. Kufuatia mzozano huo mawaziri wawili kutoka Pwani; Joho na Mvurya, wameonekana kila mmoja akijigamba kuwa kiongozi wa Wapwani. Hivi karibuni walionekana wakizozana baada ya Joho kusema kiti cha Naibu Rais mnamo 2027 lazima kiachiwe chama cha ODM kutokana na makubaliano yao ya handisheki. Waziri Joho aliye na ushawishi mkubwa Pwani ameonekana kupata uungwaji mkono wa wabunge wengi kuhusiana na azma yake ya kuwa Naibu Rais. Hata hivyo, Waziri Mvurya alijitokeza kukemea Joho na kundi lake akisema ni Rais Ruto ataamua nani atakuwa mgombea mwenza wake hivyo ODM isimtie presha.
Go to News Site