LA TAIFA LEO
RAIS William Ruto amekanusha vikali madai ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kwamba Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) itaporomoka katika miezi sita ijayo, akiyahusisha na uchawi. Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi mnamo Jumatano alipokutana na wanachama wa Shirika la Maendeleo ya Wanawake, Rais alitetea mpango huo wa bima ya afya akisisitiza kwamba unafanya kazi na kunufaisha mamilioni ya Wakenya. “Hata nasikia mwingine alisema juzi ati ana habari kwamba SHA itaporomoka ndani ya miezi sita. Kwa sababu mimi ni Rais nilijaribu kuchunguza hii habari alitoa wapi. Nikagundua alienda akaongea na waganga na wachawi wakamwambia hivyo,” alisema na kusisitiza wakosoaji wa mpango huo wanapiga tu siasa. “Leo Wakenya 30 milioni wamejisajili SHA. Kwa mwaka mmoja tumelipa hospitali Sh121 bilioni, kiwango cha juu zaidi katika historia ya nchi,” akaongeza. Rais alisema zaidi ya Wakenya30 milioni tayari wamejisajili katika SHA, hatua aliyotaja kuwa mafanikio makubwa katika juhudi za kufikia huduma ya afya kwa wote. Alifichua kuwa serikali imelipa hospitali Sh121 bilioni ndani ya mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa mpango huo—kiasi kikubwa zaidi kuwahi kulipwa kwa vituo vya afya nchini. “Leo Wakenya milioni 30 wamejisajili kwenye SHA. Kwa mwaka mmoja tumelipa Sh121 bilioni kwa hospitali, kiwango cha juu zaidi katika historia ya nchi,” alisema. Aliwalaumu wakosoaji kwa kusambaza habari potofu kwa sababu za kisiasa, akidai baadhi yao hawajasajiliwa wala kuelewa mpango huo. Gachagua alikuwa ameonya kuwa SHA iko hatarini kuporomoka katika muda mfupi ujao iwapo changamoto zinazoiandama hazitashughulikiwa haraka upesi. Akizungumza kwenye ibada ya kanisa katika Kaunti ya Kirinyaga, Gachagua alisema ana taarifa za kuaminika kuwa mfumo huo unakumbwa na matatizo makubwa ya kifedha yanayoweza kusababisha sekta ya afya kukwama. “Kuna changamoto kubwa sana katika hospitali zetu. Nina taarifa kuwa SHA inaweza kuporomoka ndani ya miezi sita ijayo, na kutakuwa na mgogoro mkubwa wa afya ambao hatujawahi kushuhudia,” alidai. Aliongeza kwamba kucheleweshwa kwa malipo ya hospitali kumeanza kuathiri utoaji huduma za afya huku baadhi ya vituo vikikumbwa na uhaba wa dawa na vifaa muhimu vya matibabu. Gachagua alionya kuwa endapo hali hiyo itaendelea basi wananchi wengi wataathirika kwani hawataweza kupata huduma bora licha ya kujisajili katika bima hiyo.
Go to News Site