LA TAIFA LEO
LUGHA ya Kiswahili huzingatia nafsi tatu katika umoja na wingi. Nafsi ya kwanza ni mimi, wingi wake ni sisi. Nafsi ya pili ni wewe, wingi ni nyinyi. Nayo nafsi ya tatu ni yeye, katika wingi ni wao. Ili kutunga sentensi sahihi, sharti tuzingatie nafsi hizi ipasavyo. Viambishi nafsi hutumiwa kuwakilisha nafsi inayozungumziwa. Mfano: Kiambishi nafsi cha nafsi ya kwanza mimi ni ni-. Kiambishi nafsi cha sisi ni tu-. Japo kutumia viambishi nafsi katika sentensi ni rahisi, kuna baadhi ya wanafunzi wenye mazoea ya kutumia nafsi pamoja na kiambishi chake katika sentensi. Aghalabu utapata sentensi kama vile: Mimi nitaenda kumtembelea mjomba kesho. Sisi tutasafisha madarasa yetu jioni. Nyinyi mliwasaidia wakulima hao kupanda miche mashambani mwao. Yeye amewapikia wageni chakula kitamu. Sentensi hizi zimetumia nafsi pamoja na viambishi vyake. Hatufai kutumia nafsi pamoja na kiambishi chake. Kutumia kiambishi nafsi pekee kumetosha kuwasilisha ujumbe katika sentensi. Ili kuzisahihisha sentensi hizi tunafaa kuondoa nafsi mimi, sisi, nyinyi, yeye na kutumia viambishi nafsi pekee. Kwa hivyo tunafaa kusema: Nitaenda kumtembelea mjomba kesho. Tutasafisha madarasa yetu jioni. Mliwasaidia wakulima hao kupanda miche mashambani mwao. Amewapikia wageni chakula kitamu. Mwanafunzi mwenye changamoto ya kutumia nafsi yoyote pamoja na kiambishi chake katika sentensi moja, afanye mazoezi ya kuandika sentensi mbalimbali kwa kutumia viwakilishi nafsi pekee.
Go to News Site