Mwananchi
Siha. Watu wanane wamenusurika kusombwa na mafuriko katika Kijiji cha Koboko Kusini, kata ya Nasai, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro baada ya nyumba zao kuzingirwa na mafuriko yaliyotokana na mvua zinazonyesha katika maeneo mbalimbali wilayani humo. Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani humo, Jeremiah Mkomagi amethibitisha kuokolewa kwa watu hao ambapo amesema mafuriko hayo yametokea leo Jumamosi asubuhi Aprili 11, 2026 wilayani humo, kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha wilayani humo. "Leo Aprili 11 2026 saa 07:45 asubuhi Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kituo cha Siha tulipokea taarifa ya tukio la maji kuzingira katika makazi ya watu (mafuriko) katika Kijiji cha Koboko kusini, Kata ya Nasai, ambapo tulifika mara moja eneo la tukio na kukuta mafuriko yamezingira makazi ya watu," amesema Kamanda Mkomagi. Kamanda Mkomagi amesema, baada ya kufika eneo la tukio askari wa jeshi hilo, walianza kazi ya kuwatoa watu waliozingirwa na maji ndani ambapo walifanikiwa kuwaokoa watu nane wakiwemo watoto sita na watu wazima wawili ambao walikuwa wamekwama ndani ya nyumba zao kutokana na mafuriko hayo. Aidha, Kamanda Mkomagi amesema katika tukio hilo hakuna vifo wala majeruhi na kwamba vitu vilivyokuwemo ndani ikiwemo magodoro, vyombo vya kupikia, majiko pamoja na vifaa vingine vimeharibiwa na mafuriko hayo. "Jeshi limefanikiwa kuokoa jumla ya watu nane wakiwemo watu wazima wawili, wote Jinsia ya kike pamoja na watoto sita ambao wote ni jinsia ya kike, ambapo idadi kamili ya kaya zillifanikiwa kuokolewa ni jumla ya kaya nne," amesema Kamanda Mkomagi. Aidha, amesema chanzo cha mafuriko hayo ni kutokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia leo na kusababisha maji kuingia katika makazi ya wananachi.
Go to News Site