LA TAIFA LEO
NAIBU Rais Profesa Kithure Kindiki alitumia Sh153.6 milioni kwa safari za helikopta kote nchini ndani ya siku 75 katika kipindi cha mwaka mmoja, kulingana na stakabadhi kutoka afisi yake zilizowasilishwa bungeni. Ufichuzi huo unajiri siku chache baada ya wabunge kuidhinisha kwa kauli moja nyongeza ya Sh450 milioni kwa Afisi ya Naibu Rais chini ya makadirio ya ziada ya bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26, fedha zilizotengwa kwa ukarimu na ukodishaji wa helikopta. Stakabadhi hizo, zilizowasilishwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Umma, zilikuwa majibu kwa maswali ya ukaguzi kuhusu hesabu za mwaka wa fedha 2023/24. Ziliwasilishwa na Katibu Mkuu Tawala Moses Mbaruku. Kulingana na majibu hayo, Wakenya pia walitumia Sh117.3 milioni kwa huduma za upishi, Sh80.24 milioni kwa kukodisha mahema na mapambo, na Sh40.4 milioni kwa ununuzi wa vyakula, ikiwemo nafaka, nyama, mboga na kabichi kwa matumizi ya afisi ya Naibu Rais. Cha kushangasha, matumizi haya makubwa ya helikopta yanajiri wakati Rais William Ruto ametangaza hatua za kubana matumizi serikalini, huku Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kenya ikiendelea kukosa kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato, hali inayochochea ongezeko la deni la umma. Wanachama wa kamati hiyo wakiongozwa na Mbunge wa Rarieda Dkt Otiende Amollo walihoji matumizi hayo, wakishangazwa na matumizi ya hadi Sh8 milioni kwa siku moja katika safari za helikopta mara mbili tofauti. “Je, ni busara kutumia Sh8 milioni kwa siku moja kwa safari za helikopta? Hili linawezekana kweli?” alihoji Dkt Amollo. Stakabadhi kutoka afisi ya Naibu Rais hazikueleza wazi shughuli alizokuwa akifanya wakati wa safari hizo. Hata hivyo, muda wa safari hizo unaonekana kuendana na maandalizi ya uchaguzi mdogo wa Novemba 27, 2025 katika maeneo 24 ya uchaguzi, ambapo chama tawala kilikuwa kinapania kushinda. Kwa mfano, Juni 25 2025, Naibu Rais alitumia Sh8.2 milioni kwa siku moja kwa safari zilizohusisha maeneo ya Chepsaita, Eldoret, Kipkaren, Kisii, Webuye, Bomet na Baringo. Malipo yalifanywa Novemba 17, 2025. Katika tukio jingine, alitumia Sh8.1 milioni kwa safari katika kaunti za Tharaka, Laikipia, Isiolo na Kitui, huku malipo yakifanywa Septemba 15, 2025. Mnamo Julai 2, 2025, alitumia Sh6.9 milioni kwa safari zilizohusisha Isiolo, Mombasa, Malindi, Kilifi, Voi na Kanyuambora. Aidha, Februari 24, 2025, alitumia Sh4.1 milioni kwa safari katika kaunti za Mombasa na Kilifi. Matumizi mengine ni pamoja na Sh3.8 milioni kwa safari za Magarini, Malindi, Voi na Taita, pamoja na Sh3.45 milioni kwa safari za Embu, Tharaka, Nanyuki, Kisumu na Homa Bay. Mbunge wa Funyula Dkt Wilberforce Oundo alikosoa matumizi hayo, akiyataja kuwa hayana hisia kwa hali ya uchumi wa wananchi.
Go to News Site