Collector
Kuibuka kwa magenge ya wahuni kunaakisi roho ya uongozi nchini | Collector
Kuibuka kwa magenge ya wahuni kunaakisi roho ya uongozi nchini
LA TAIFA LEO

Kuibuka kwa magenge ya wahuni kunaakisi roho ya uongozi nchini

KUIBUKA kwa magenge ya wahuni katika mikutano ya kisiasa na maandamano si bahati mbaya, bali ni kielelezo cha hali ya uongozi nchini. Pale ambapo viongozi wanatumia lugha ya chuki, vitisho na misimamo mikali ya kisiasa, wanachochea mazingira yanayoruhusu vurugu kustawi. Magenge haya hayazaliwi tu mitaani; mara nyingi huwa kivuli cha siasa zisizo na uwajibikaji. Ni wazi kuwa wahuni wanaovamia mikutano, kuharibu mali na kuwadhulumu wananchi hawafanyi hivyo kwa hiari yao pekee. Mara nyingi kuna mkono wa kisiasa nyuma yao—ama kwa kuwachochea, kuwafadhili au kuwapa kinga. Hii inaonyesha kuwa tatizo si la usalama pekee, bali ni la maadili ya uongozi. Hatari yake ni kubwa. Kwanza, inavuruga utawala wa sheria. Wananchi wanaposhuhudia wahuni wakitenda uhalifu bila kuchukuliwa hatua, imani yao kwa taasisi za serikali hupungua. Pili, inahatarisha maisha na mali ya watu wasio na hatia. Biashara huporwa, watu hujeruhiwa na wengine kupoteza maisha katika vurugu ambazo zingeweza kuepukika. Zaidi ya hayo, tabia hii inajenga utamaduni hatari wa kisiasa ambapo nguvu na hofu zinachukua nafasi ya hoja na sera. Vijana, badala ya kushirikishwa katika ujenzi wa taifa, wanageuzwa zana za vurugu kwa manufaa ya wanasiasa. Hili ni pigo kwa mustakabali wa nchi. Serikali na viongozi wa kisiasa lazima wawajibike. Ni lazima kuwe na msimamo thabiti dhidi ya ufadhili na matumizi ya magenge ya wahuni. Viongozi wanapaswa kuonyesha mfano kwa kuhubiri amani na kuheshimu sheria, badala ya kuchochea mgawanyiko. Roho ya magenge ya wahuni inaakisi moja kwa moja roho ya uongozi. Ikiwa uongozi utakuwa wa vurugu na hila, jamii nayo itafuata mkondo huo. Lakini ikiwa uongozi utasimama katika haki, uwajibikaji na amani, basi hata wananchi wataiga. Bila hatua za haraka, mwenendo huu unaweza kupeleka nchi katika hatari kubwa ya kuyumba kwa utulivu na mshikamano wa kitaifa.

Go to News Site