Collector
Kila kitu kiko shwari; hatuwezi kukosana, Ruto ahakikishia ODM | Collector
Kila kitu kiko shwari; hatuwezi kukosana, Ruto ahakikishia ODM
LA TAIFA LEO

Kila kitu kiko shwari; hatuwezi kukosana, Ruto ahakikishia ODM

RAIS Ruto amewalaumu baadhi ya wanasiasa kwa kukubali kutumiwa kuzua mgawanyiko huku akisisitiza kuwa ushirikiano wa UDA na ODM utadumu hata baada ya uchaguzi mkuu wa 2027. Rais amelazimika kuingilia suala hilo baada ya baadhi ya wanasiasa wa ODM kudai kuwa wenzao wa UDA wanatumia ushirikiano wao na serikali kulemaza chama hicho cha Chungwa. Baadhi ya wabunge kutoka mrengo wa Linda Mwananchi ndani ya ODM wametofautiana na kauli ya Kiongozi wa Wachache katika Bunge, Junet Mohamed kuwa baadhi ya viongozi wa UDA serikalini wanatumia vyombo vya serikali kukandamiza ODM. Bw Mohamed alidai kuwa baadhi ya wabunge wa ODM sasa wanalazimishwa kujiunga na UDA kuelekea kura ya 2027. Bw Mohamed, inaonekana anaungwa mkono na Gavana wa Homa Bay, Gladys Wanga ambaye amekuwa akisisitiza kuwa ODM itengewe ngome zake za kisiasa kutokana na muafaka wake na UDA. Baadhi ya wanasiasa wa ODM wamemtaja Naibu Rais Prof Kithure Kindiki na Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani Raymond Omollo wakisema wanatumia nyadhifa zao kukandamiza ODM. Kamati simamizi ya ODM ilipanga kuandaa mkutano wake jana kuzungumzia uhusiano kati yao na UDA lakini kikao hicho kikaahirishwa hadi Aprili 16. Bw Mohamed alisema wanachama wengi hawakuwepo Nairobi. Baadhi ya wanachama wa ODM sasa wanamtaka Dkt Oginga achukue hatua na msimamo mkali wanapojadiliana na UDA. Jana akiwa eneo la Gusii, Rais Ruto alihakikishia ODM kuwa kila kitu ki shwari wala hatakubali watu wachache wasambaratishe uhusiano wa chama hicho na UDA. “Wale ambao wanajaribu kugonganisha ODM na UDA, nitawazima kwa sababu sitaki mgawanyiko ndani ya vyama vyetu,” akasema Rais Ruto. Alionekana kumjibu Gavana wa Kisii Simba Arati ambaye alikuwa amemtaka aingilie kati kuzima tofauti zinazoendelea kuchipuka kati ya UDA na ODM. “Tutaendelea kushirikiana na UDA jinsi alivyoamrisha Baba Raila Odinga. Hata hivyo, nataka nikwambie kuna tatizo upande wa UDA. Wazime ili tuendelee kufanya kazi pamoja,” akasema Bw Arati. Mnamo Jumatatu, Rais Ruto alichapisha kwenye mtandao wa X kuhusu suala hilo akilaumu wanasiasa ambao hakuwataja kwa kuhusika na mgongano huo. “UDA na ODM zitaendelea kufanya kazi pamoja na wale wanaotumiwa kuzua mgawanyiko hawatafaulu. Nchi yetu ni bora, ODM na UDA zikifanya kazi pamoja,” akasema Rais Ruto. Rais alisisitiza kuwa haikuwa bahati au kimakosa kushirikiana na marehemu Raila aliyeaga dunia Oktoba 2025. “Tulipounda serikali hii haikuwa kwa kosa, tulikuwa na nia. Nilitaka hali ambapo hakuna Mkenya anayeachwa nje na ni matumaini yangu kuwa Serikali Jumuishi itawaleta watu pamoja,” akasema. Mnamo Jumatatu baadhi ya wabunge wa ODM walikuwa wamepanga kuandaa mkutano kukashifu matamshi ya Bw Mohamed lakini mkutano huo ukaahirishwa kwa sababu wabunge wengi hawakuwa Nairobi. Kikao kingine kilichokuwa kiandaliwe Jumanne nacho pia kiliahirishwa huku duru zikiarifu kuwa suala hilo litazungumziwa kwenye kikao kitakachoongozwa na Dkt Oginga. “Ni kiongozi wa chama pekee anastahili kutoa msimao wa chama au katibu mkuu na kwa mujibu wa kiongozi wa chama, ODM inasalia ndani ya Serikali Jumuishi. Hakuna ushahidi kuwa wanachama wetu wanahangaishwa au kulazimishiwa mambo,” akasema Mbunge wa Gem, Elisha Odhiambo. Mbunge wa Uriri, Mark Nyamita alisema uhusiano na UDA ndio bora zaidi kwa ODM kwa sasa huku akipuuza madai kuwa kuna kutoaminiana. “Miungano mingine haina nafasi katika eneo letu na hii Serikali Jumuishi, tumeona matunda yake,” akasema Bw Nyamita. Bi Wanga amekuwa akisisitiza kuwa hata kama ODM inashirikiana na UDA lazima isalie na utambulisho wake na lazima iachiwe ngome zake za kisiasa. Wabunge Otiende Amollo (Rarieda) na Beatrice Elachi (Dagoretti Kaskazini) nao wametoa wito wa kubuniwa kwa kamati ya kuongoza mazungumzo kati ya UDA na ODM ili kutatua tofauti zinazoibuka kuhusu masuala tata.

Go to News Site