Collector
Ni kubaya, kaza mshipi wako; bei za mafuta zaweza kuleta masaibu mapya ya kiuchumi | Collector
Ni kubaya, kaza mshipi wako; bei za mafuta zaweza kuleta masaibu mapya ya kiuchumi
LA TAIFA LEO

Ni kubaya, kaza mshipi wako; bei za mafuta zaweza kuleta masaibu mapya ya kiuchumi

WAKENYA waliamkia wimbi jipya la masaibu kiuchumi hapo jana huku wakianza kuhisi athari za bei za mafuta kuongezwa, hali iliyosababisha nauli, bei ya vyakula, na gharama ya huduma muhimu kote nchini kupanda ghafla. Ongezeko hilo la kihistoria lililotangazwa na Mamlaka ya Kawi na Petroli (EPRA), limevuruga mfumo wa uchumi huku wasafirishaji, wafanyabiashara na watoaji huduma wakipitisha upesi gharama ya ziada kwa wanunuzi bidhaa ambao tayari wanatatizika na gharama ya juu ya maisha. Katika tangazo la bei mpya, Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Petroli (EPRA) iliongeza lita ya petroli kwa Sh28 na dizeli Sh40. Mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki wa Matatu (MOA) Albert Karakacha, alitangaza nyongeza ya asilimia 25 kwa nauli kote nchini kugharimia bei ghali ya mafuta. “Tumeshauriana na kuafikiana kuwa tutaongeza bei kwa asilimia 25 kote nchini ili tujikinge. Tunahimiza wateja wetu, ambao ni umma kwamba si lengo letu kuchukua mwelekeo huo. Tuko kwenye biashara na ni sharti watustahimili,” alisema Bw Karakacha. “Nyongeza ya nauli na ada nyinginezo ilikuwa jibu la papo hapo kwa bei mpya za mafuta. Tunatathmini athari na tutatangaza mikakati zaidi baadaye,” alisema Bw Reuben Donga, naibu mwenyekiti wa shirika la 2NK Sacco, linaloendesha shughuli zake maeneo ya Kati na Bonde la Ufa. Gharama ya kusafirisha shehena kutoka Bandari ya Mombasa kuelekea Nairobi na sehemu nyingine imepanda pakubwa vilevile, ambapo gharama ya ziada inatarajiwa kupitishwa kwa wanunuzi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nchi za kigeni. Mwenyekiti wa Muungano wa Wasafirishaji nchini (KTA), Newton Wang’oo alisema gharama ya kusafirisha mizigo kote nchini itaongezeka kwa karibu asilimia 14 kuanzia jana. Kusafirisha kontena ya futi 20 kutoka Mombasa hadi Nairobi sasa itagharimu Sh130,000, kutoka Sh115,000, huku kontena ya futi 40 ikigharimu Sh142,000, kutoka Sh119,000. KTA, inayowakilisha zaidi ya matrela 6,000 ya kusafirisha mizigo kote nchini, ilisema wanachama wake hawawezi kustahimili gharama ya ziada na itaipitisha kwa wanunuzi bidhaa. Muungano wa Matrela (TAK) umeagiza wanachama wake kuongeza ada za usafirishaji kwa asilimia 30, ukitaja ongezeko la bei ya mafuta. Wahudumu katika usafiri wa umma yakiwemo mashirika ya matatu wameongeza nauli vilevile kwa kati ya asilimia 30 na 50. Nauli kutoka Meru hadi Nairobi imeongezeka kutoka Sh1,200 hadi kati ya Sh1,500 na Sh2,000, kulingana na Katibu wa Muungano wa Wamiliki Matatu Meru, Joseph Bundi. Murang’a, wasafirishaji wa vifaa vya ujenzi wameongeza ada zao kwa kati ya asilimia 30 na 50, hatua inayotarajiwa kupandisha gharama ya makazi. Nauli kutoka Nairobi hadi Murang’a imeongezeka hadi kufikia kati ya Sh350 na Sh400, kutoka Sh300, huku abiria wanaosafiri kati ya Thika na Murang’a sasa wakilipa Sh250, kutoka Sh150. Nakuru, wasafiri katika mikondo kadhaa mjini sasa wanalipa Sh70 kutoka Sh50. Katika soko la Wakulima, bei ya vitunguu imepanda kutoka Sh100 hadi Sh130 kwa kila kilogramu. Wanaosafiri kutoka Bomet hadi Eldoret sasa wanalipa Sh1,000, kutoka Sh900, huku wanaosafiri kuelekea Nairobi vilevile wakilipa Sh1,000. Narok Kusini na Emurua Dikirr, nauli zimepanda kutoka Sh500 hadi Sh700 kwenye baadhi ya mikondo na mingine ikipanda kutoka Sh300 hadi Sh500. Kaunti za Nyandarua na Laikipia, wanaosafiri kutoka Ol Kalou kuelekea Nyahururu sasa wanalipa Sh200, kutoka Sh150, huku wanaosafiri kati ya Nyahururu na Nakuru wakilipa Sh400 kutoka Sh300. Wakulima katika kaunti za Uasin Gishu, Trans Nzoia na Nandi wanasema ongezeko la bei za mafuta limezidisha gharama ya kilimo cha mashine. Dizeli inayoendesha trekta na mashine za kuvuna imekuwa ghali mno. Lodwar, Turkana, waendeshaji bodaboda wameachisha kazi pikipiki zao wakitaja bei ghali za mafuta wakisema wateja wanajiepusha kusafiri kutokana na nauli zisizotabirika. Kabarnet na Baringo, bei za mafuta zilipanda kutoka Sh179 hadi Sh207 kwa lita. Kitale na sehemu za Trans Nzoia, vituo vingi vya mafuta vilitekeleza bei mpya kufikia leo asubuhi, huku petroli na dizeli zikiuzwa kwa Sh207 kwa kila lita. Nyanza Kusini, wamiliki wa matatu walisema watabadilisha nauli wakijitahidi kusawazisha kati ya kulinda wasafiri na kust awisha oparesheni zao. Msimamizi wa shirika la Busia, Kisumu na Migori (BUKIMI), Joshua Ouma, alisema nauli itabadilishwa kuambatana na bei mpya za mafuta.

Go to News Site