LA TAIFA LEO
MAAFISA wa upelelezi kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wameelekeza uchunguzi wao kwenye simu za mkononi na taarifa za benki zilizopatikana kutoka kwa washukiwa wanne waliokamatwa Diani kuhusu msururu wa wizi wa kimabavu katika kaunti tatu. Uchambuzi wa vitu hivyo vitasaidia DCI kufumbua kitendawili cha msururu wa wizi wa kimabavu ambayo pia imechangia maafa ya baadhi za waathiriwa katika kesi hiyo. Washukiwa hao, Bernard Mbusu, Isaac Kinoti Kobia, Evan Muthengi Mutaki na Kelvin Mwangi Njoroge wanatuhumiwa kutekeleza vitendo hivyo katika kaunti za Mombasa, Nairobi na Kilifi. Wanne hao pia wanachunguzwa kuhusiana na mauaji ya mfanyabiashara raia wa Scotland Campbell Scott, ambaye mwili wake ulipatikana ndani ya gunia mwaka jana. Siku ya Jumatatu, Mahakama ya Shanzu iliruhusu polisi kuwazuia washukiwa hao kwa siku 14 ili kukamilisha uchunguzi. Kulingana na maombi yaliyowasilishwa mahakamani, afisa wa uchunguzi Sajenti Fredrick Ochido alisema washukiwa hao walikamatwa katika makazi ya Deal Apartments, Ukunda, Kaunti ya Kwale, Aprili 11, 2026 saa tatu na robo usiku, na baadaye kufikishwa katika kituo cha polisi cha Nyali. Aliiambia mahakama kuwa washukiwa hao wanahusishwa na uhalifu mbalimbali katika maeneo tofauti, ikiwemo wizi wa kimabavu kilichoripotiwa katika Kituo cha polisi cha Watamu, Kaunti ya Kilifi, chini ya OB nambari 45 /2/13/ 2026. Pia wanachunguzwa kwa kosa la mauaji kinyume kufuatia tukio lililoripotiwa katika kituo cha lolisi cha Parklands jijini Nairobi chini ya OB nambari 14/2/17/ 2026. Aidha, wanahusishwa na tukio jingine la wizi wa kimabavu lililoripotiwa katika kituo cha polisi cha Nyali, Kaunti ya Mombasa, chini ya OB nambari 58/4/ 9/ 2026. Wapelezi waliieleza mahakama kuwa wanahitaji muda zaidi kuwasilisha simu za washukiwa hao katika maabara ya uchunguzi wa kielektroniki makao makuu ya DCI jijini Nairobi kwa uchambuzi. Pia, walisema wanapanga kupata rekodi za mawasiliano ya simu, taarifa za M-Pesa pamoja na taarifa za akaunti za benki ili kusaidia uchunguzi. Kwa mujibu wa stakabadhi zilizowasilishwa Mahakamani, wapelelezi wanatafuta pia picha za kamera za ulinzi kutoka maeneo ya uhalifu na mashine za kutoa pesa za benki ambako washukiwa hao wanadaiwa kutumia kadi za benki za mlalamishi kutoa fedha, ili zichunguzwe kitaalamu. "Mlalamishi, ambaye ni raia wa Marekani, bado hajashiriki katika gwaride la utambuzi wala kutambua mali zilizopatikana wakati wa uchunguzi," polisi walisema. Mahakama iliambiwa kuwa zoezi hilo litafanyika katika kituo cha polisi cha Nyali. Polisi pia waliieleza mahakama kuwa bado hawajakusanya taarifa kutoka kwa mashahidi muhimu. Bw Ochido alisema muda uliopita tangu washukiwa wakamatwe hautoshi kukamilisha uchunguzi na kuamua iwapo watafunguliwa mashtaka. Aliomba mahakama iruhusu washukiwa hao kuzuiliwa katika vituo vya polisi vya Nyali na Kadzandani kwa siku 15 ili uchunguzi ukamilishwe na hatua mwafaka zichukuliwe. Katika taarifa iliyotolewa baada ya kukamatwa kwao, DCI ilisema operesheni hiyo ilifanyika kufuatia upelelezi wa kina ulioshirikisha idara mbalimbali, ukiwahusisha maafisa kutoka Kitengo cha Utafiti wa Uhalifu na Ujasusi kwa kushirikiana na wenzao wa Nyali na Msambweni. DCI lilisema kukamatwa kwa washukiwa hao kunahusishwa na uchunguzi wa visa vya wizi wa kimabavu dhidi ya raia wa Marekani huko Nyali pamoja na utekaji nyara na mauaji ya raia wa Uingereza, Scott, yaliyotokea Februari 2025, ambayo mwili wake ulipatikana Mukuyuni kando ya barabara ya Machakos kuelekea Wote. Wapelelezi waliongeza kuwa ushahidi wa kitaalamu umeonyesha pia kuwa washukiwa hao wanahusishwa na tukio jingine la wizi wa kimabavu lililotokea Watamu, eneo la Malindi. Upekuzi uliofanywa katika makazi yao ulisababisha kupatikana kwa mali zinazodaiwa kuibwa, zikiwemo kompyuta aina ya HP, simu za mkononi, fedha za kigeni, kadi mbalimbali za benki, vitabu vya hundi kutoka taasisi tofauti za kifedha pamoja na mashine za malipo ya kielektroniki. Polisi wanasema vifaa hivyo vitasaidia kubaini kwa kina mtandao wa wizi wa kimabavu na kuwafahamu waathiriwa wa msururu wa uhalifu. Scott alikuwa amewasili Nairobi Februari 2025 kuhudhuria mkutano wa kibiashara na alikuwa akiishi Westlands, lakini alitoweka baada ya kukosa kuhudhuria kikao muhimu na wenzake. Uchunguzi ulionyesha kuwa mara ya mwisho alionekana katika klabu moja ya burudani jijini kabla ya kudanganywa na kupelekwa katika nyumba moja eneo la Pipeline, ambako inaaminika alizuiliwa huku wahalifu wakijaribu kupata fedha kutoka kwenye akaunti zake za benki. Baadaye mwili wake ulipatikana umefungwa ndani ya gunia na kutupwa katika msitu wa Makongo, Kaunti ya Makueni, siku kadhaa baada ya kutoweka.
Go to News Site