Collector
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Adhabu kwa mafisadi iko dhahiri kwa Waislamu, ni kali | Collector
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Adhabu kwa mafisadi iko dhahiri kwa Waislamu, ni kali
LA TAIFA LEO

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Adhabu kwa mafisadi iko dhahiri kwa Waislamu, ni kali

BISMILLAHI rahman raheem alhamdulillahi rabbil alamin. Kama kawaida ya kila Ijumaa, Allah (SWT) ametutunuku uhai ili tuendelee kujifunza mambo mengi kuhusu Dini yetu tukufu ya Kiislamu. Leo jinsi tunavyoshaajishana kila Ijumaa, ni vyema tufike msikiti kuwahi swala na pia kusikiza hotuba na mafunzo ya Maimamu, mashekhe, maulamaa na wasomi wengine wa dini. Mafunzo haya yana umuhimu kuyaongoza maisha yetu ndani ya sayari hii. Kabla ya kuzamia mada ya leo, kama ada tuanze kwa kumshukuru mno Muumba wetu Subuhaanahu wata’ala, mwingi wa rehema na muumba wa mbingu na ardhi na vyote vilivyomo. Kila siku hata milele hapana mwingine anayestahili kuabudiwa na kuenziwa ila ni Allah (SWT) pekee. Baada ya kumshukuru Allah (SWT) wetu, pia tuchukue muda huu wa kipekee kumtakia kheri, kumtilia dua na kumfanyia maombi kipenzi chetu Mtume wetu Mohamed (SAW). Ni vyema tushukuru Allah kwa uhai licha ya kwamba kwa sasa taifa letu linakumbwa na changamoto kadhaa za kiuchumi. Kinywani mwa kila mja ni kupanda kwa bei ya mafuta na maisha magumu ambayo yanawakodolea raia macho ndugu yangu, leo katika safu hii naomba tuzungumzie ufisadi ambao ndio umesakama idara mbalimbali za serikali na kutikisa uchumi wetu. Kwa sasa kumetanda lawama kotekote miongoni mwa wanasiasa wetu baada ya kuibuka kwa sakata ya mafuta nchini. Quran inakemea ‘fasad’ na Surah Al Qasas 28:77 inasema “Usiwe na tamaa ya fasad ulimwenguni, hakika Allah hapendi wafisadi”. Allah ameweka makundi manne ya ufisadi mmoja ikiwa ni tamaa ya fedha ambayo inashirikisha utoaji hongo, kupata mali kwa njia ya ulaghai na kushiriki hadaa kwenye biashara. Aina ya pili ya fasad ambayo Allah ameharamisha ni kutumia mamlaka vibaya hasa kwa viongozi ambao wanawadhulumu na kuwafanya watumwa wale ambao wamewachagua raia. Mwenyezi Mungu pia hataki ghasia na umwagikaji wa damu. Kushiriki mauaji au kuharibu mali kunachukuliwa kama kutangaza vita dhidi ya Allah. Kisha aina ya nne ya ufisadi ni ukosefu wa maadili katika jamii ambao unahusisha unafiki na pia usaliti. Ukitathmini aina hizi zote za ufisadi basi hakuna hata mmoja ambayo viongozi wetu nchini wamekosa kushiriki. Yaani wanaogolea na kutopea katika bahari ya ufisadi. Kila leo huwa ni kufuja tu mali ya umma huku viongozi wakizidi kuwa matajiri, wanakula na kusaza nao wananchi wakiendelea kuandamwa na umaskini mkubwa. Kwa wafisadi Surah Al-Baqarah 2:85 inawaambia “Siku ya ufufuo wataangushiwa adhabu kali tena baya zaidi”. Surah Al-Ma’idah 5:33 nayo inaweka mambo paruwanja zaidi kwa wafisadi “Watauawa, kusulubishwa, mikono na migu yao itakatwa au watafurushwa kuishi uhamishoni.” Kabla ya kupora mali ya umma, kiongozi afahamu kuna adhabu inayomsubiri.

Go to News Site