Collector
Uelewa mdogo wa jamii unavyotishia janga la glaucoma | Collector
Uelewa mdogo wa jamii unavyotishia janga la glaucoma
Mwananchi

Uelewa mdogo wa jamii unavyotishia janga la glaucoma

Katika jamii yetu, bado kuna baadhi ya magonjwa ambayo hayapati uzito unaostahili. Hali hii inachangiwa na sababu mbalimbali, ikiwemo ukweli kwamba mara nyingi huathiri zaidi watu wa kipato cha chini, dalili zake hujitokeza taratibu bila kuonekana kama dharura, pamoja na ukosefu wa elimu ya afya kwa jamii na uhaba wa rasilimali katika sekta ya afya nchini. Kwa kawaida, magonjwa yanayopewa kipaumbele ni yale yanayosababisha vifo vingi, yanayoenea kwa kasi au kuwa na athari kubwa kwa jamii. Miongoni mwa magonjwa hayo ni Virusi vya Ukimwi, saratani, shinikizo la damu, kifua kikuu, malaria na kisukari; magonjwa ambayo kwa kiasi kikubwa yamejengewa taswira ya kuwa hatari zaidi. Hata hivyo, hali hiyo imeifanya jamii kusahau uwepo wa magonjwa mengine muhimu, yakiwemo ya macho, ngozi, pamoja na yale ya koo, pua na sikio. Magonjwa haya nayo yameendelea kuwa tatizo kubwa nchini, hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya sayansi na teknolojia. Katika makala hii, tunaangazia ugonjwa wa shinikizo la macho (glaucoma), ambao ni miongoni mwa magonjwa hatari ya macho yanayoweza kusababisha upofu wa kudumu endapo hayatagunduliwa na kutibiwa mapema. Habari njema ni kwamba ugonjwa huu unaweza kudhibitiwa iwapo utabainika mapema. Daktari bingwa wa macho, Dk Gazilo Zacharia wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora (Kitete), anaeleza kuwa glaucoma ni kundi la magonjwa yanayoharibu neva ya macho (optic nerve), ambayo husafirisha taarifa za kuona kwenda kwenye ubongo. Mara nyingi, uharibifu huu husababishwa na kuongezeka kwa shinikizo ndani ya jicho. “Ndani ya jicho kuna maji maalum yanayoitwa 'aqueous humor'. Maji haya hutengenezwa kila wakati na hutoka kupitia njia maalum. Njia hizi zinapoziba au kushindwa kufanya kazi ipasavyo, maji hukusanyika na kuongeza shinikizo ndani ya jicho, hali inayosababisha uharibifu wa neva ya macho,” anaeleza. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kupitia taarifa yake ya mwaka 2026 (ikiwa na takwimu za 2025), glaucoma ni miongoni mwa visababishi vikuu vya upofu duniani. Inakadiriwa kuwa watu milioni 7.7 wanakabiliwa na ulemavu wa kuona au upofu unaotokana na ugonjwa huo. Hali hii inaweka wazi ukubwa wa tatizo hilo kimataifa, sambamba na magonjwa mengine ya macho kama mtoto wa jicho (cataract). Utafiti wa Mahenge Utafiti uliofanyika Mahenge, mkoani Morogoro, unaonesha ukubwa wa tatizo hilo nchini, ambapo asilimia 33 ya watu waliochunguzwa walibainika kuwa na dalili za glaucoma. Matokeo haya yanaashiria umuhimu wa jamii kujenga utamaduni wa kupima macho mara kwa mara, hasa kwa makundi yaliyo katika hatari kubwa. Dk Gazilo anabainisha kuwa changamoto kubwa ya glaucoma ni kutokuwa na dalili za wazi katika hatua za mwanzo. Ugonjwa huu huanza kwa kupunguza uwezo wa kuona taratibu, ambapo mgonjwa anaweza kuona kama anachungulia kupitia bomba (pipe), huku uharibifu wa neva ya macho ukiendelea kimyakimya. Kwa mujibu wa wataalamu wa afya ya macho, inapendekezwa kuwa watu wenye umri mkubwa au walio katika hatari wapime macho angalau kila baada ya mwaka mmoja hadi miwili. Wenye historia ya familia ya ugonjwa huo wanapaswa kuanza vipimo mapema zaidi, huku wagonjwa wa kisukari na shinikizo la damu wakishauriwa kufanya uchunguzi mara kwa mara. Sababu za hatari ni pamoja na historia ya kifamilia, umri (hasa kuanzia miaka 40 na kuendelea), pamoja na shinikizo kubwa ndani ya jicho. Aidha, magonjwa kama kisukari na shinikizo la damu yasiyodhibitiwa, pamoja na matatizo ya mishipa ya macho, huongeza uwezekano wa kupata glaucoma. Vilevile, watu wenye rangi ya ngozi nyeusi hususan Waafrika, wapo katika hatari kubwa zaidi. Pia, majeraha au upasuaji wa jicho vinaweza kusababisha aina nyingine ya glaucoma. Matatizo kama mtoto wa jicho mkubwa au miwasho ya mara kwa mara ya macho yanaweza kuchangia kutokea kwa glaucoma ya pembe iliyofungwa. Kutokana na ukweli kwamba glaucoma haina dalili za awali zinazoonekana kirahisi, wataalamu wanasisitiza umuhimu wa uchunguzi wa mara kwa mara wa macho, ikiwemo kupima shinikizo la jicho, kuchunguza neva ya macho na uwanja wa kuona. Vilevile, kuishi maisha yenye afya, kudhibiti presha ya damu na sukari, pamoja na kuepuka uvutaji wa sigara, ni hatua muhimu za kujikinga. Kwa upande wa kiuchumi, tafiti zinaonesha kuwa gharama ya matibabu ya glaucoma inaweza kufikia hadi asilimia 25 ya kipato cha mtu, jambo linaloweza kuwa kikwazo kikubwa kwa wengi kupata huduma stahiki. Kwa ujumla, ipo haja ya kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu ugonjwa huu hatari. Bila hatua za makusudi za elimu na uchunguzi wa mapema, glaucoma itaendelea kuwa tishio kubwa linalonyemelea afya ya macho ya Watanzania wengi.

Go to News Site