LA TAIFA LEO
MWENYEKITI wa kampuni ya Stabex International Ltd, Jackson Chebett, amemshtaki aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kumchafulia jina kwa kumhusisha na sakata ya hivi majuzi ya mafuta. Bw Chebett anasema kuwa kampuni yake haihusiki na mfumo wa serikali kwa serikali wala haina uhusiano na Rais William Ruto kama alivyodai Gachagua. Anadai kuwa kauli ya Gachagua, ambayo alirudia mara kadhaa, ilichochewa na nia mbaya, wivu wa kisiasa na uzembe, ikilenga kupotosha umma. “Haina ukweli wowote, inapuuza rekodi za umma na kwa makusudi inatumia lugha ya uchochezi ili kuchochea hasira ya wananchi kwa manufaa ya kisiasa,” inasema sehemu ya kesi hiyo. Bw Chebett anasema amejenga biashara kubwa na yenye heshima kupitia miaka mingi ya bidii, uadilifu, kutii sheria na kufuata kanuni katika sekta ya kawi na mali isiyohamishika. “Mlalamishi ni mtu mwenye heshima na amejenga sifa zake kwa bidii, uwazi na kujituma,” aliongeza. Anasema kauli ya Gachagua ilieleweka na watu wa kawaida kumaanisha kuwa mafanikio yake ya kibiashara yamepatikana kupitia ufisadi, upendeleo wa kisiasa na matumizi mabaya ya mamlaka ya serikali badala ya biashara halali. Bw Chebett alisema Stabex ni kampuni binafsi ya mafuta yenye heshima inayomiliki zaidi ya vituo 200 vya mafuta na mabohari 14 ya kuhifadhi bidhaa katika Afrika Mashariki. Pia, anasema yeye ni mkurugenzi na mwenyehisa katika kampuni ya Ultra Eureka Ltd, ambayo hivi majuzi ilinunua mali ya thamani ya aliyekuwa waziri Raphael Tuju iliyoko Karen kupitia mnada wa hadhara. Anasema kutokana na kauli za Gachagua, yeye na kampuni zake wamepata madhara makubwa ya sifa, kupoteza imani ya kibiashara, uwezekano wa kupoteza mikataba na msongo wa kihisia, akisema madhara hayo yanaendelea na hayawezi kurekebishwa bila uamuzi wa mahakama. Bw Chebett alieleza kuwa mnamo Aprili 9 aliandika barua rasmi ya kumtaka Gachagua kutoa ufafanuzi na kuomba radhi, lakini hajafanya hivyo. Anaomba mahakama kutoa amri ya kudumu kumzuia Gachagua kutoa kauli kama hizo, kumlazimisha kuziondoa na kuomba radhi hadharani.Pia anataka fidia kwa madhara ya kimaadili na kibiashara yaliyompata yeye binafsi na kampuni zake mbili.
Go to News Site