LA TAIFA LEO
MAAFISA wa polisi Lamu na Pwani wameamriwa kuwapiga risasi na kuwaua wahalifu wa magenge ya mapanga na visu, maarufu Panga Boys. Akizungumza wakati wa kikao cha baraza la usalama kisiwani Lamu Jumatano, Kamamda wa Polisi Ukanda wa Pwani, Bw Ali Nuno, alisema idara ya usalama imekuwa ikifuatilia kwa karibu wahusika wote wa magenge ya mapanga ambao wamekuwa wakihangaisha wananchi na hata kuwadhuru Lamu na Pwani na kwamba wakati umewadia kwao kumalizwa. Bw Nuno aliwataja wahalifu wa mapanga kuwa sawa na magaidi, hivyo akaamuru polisi kuhakikisha wanawapiga risasi na kuwaua yeyote atakayepatikana amebeba silaha hatari, ikiwemo mapanga na visu. "Nataka kuongea na vijana. Ninawaambia leo hii kwamba wale mnaojihusisha na uhalifu, ikiwemo kukata watu kiholela kwa mapanga tunawajua. Tuko na historia zenu na mjue hamna muda tena. Wakati wenu umekwisha," akasema Bw Nuno. Aliongeza, "Kazi kwenu sasa nyinyi maafisa wa usalama. Nataka tukitoka hapa mhakikishe yeyote anayepatilana amebeba silaha hatari, mpigeni risasi na mumwangushe yeye. Aliye na swali aniulize mimi. Pigeni wao risasi na muwamalize kwani wamemaliza watu wetu." Akigusia suala la dawa za kulevya, Bw Nuno aliamuru polisi kutekeleza upekuzi na kuwasaka wahusika wa mihadarati na kuhakikisha pia wanakamatwa na hatua kali kuchukuliwa dhidi yao. "Wahusika wa ulanguzi wa dawa za kulevya pia mjue siku zenu zimefikia kikomo. Polisi ninawataka mhakikishe hao wanaosambazia mihadarati hapa wamekamatwa na hatua kali zichukuliwe dhidi yao. Hakuna kuwabembeleza tena. Msako ufanywe barabarani,baharini, majumbani na kila mahali na kuhakikisha wahusika wote wa ulanguzi wa dawa za kulevya wanatiwa mbaroni," akasema Bw Nuno. Idara ya Usalama Ukanda wa Pwani ikiongozwa na Mshirikishi wa Usalama eneo hilo, Bi Rhoda Onyancha na Bw Nuno imekita kambi kaunti ya Lamu kushughulikia suala la usalama, ikiwemo ongezeko la visa vya vijana kuvamiana na kuuana kwa mapanga. Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, takriban vijana 10 wameuawa kwa kukatwa na panga ilhali makumi wengine wakiachwa na majeraha mabaya. Kufikia sasa zaidi ya vijana 45 tayari wametiwa mbaroni kuhusiana na suala hilo. Kwa upande wake, Bi Onyancha aliwakashifu wazazi kwa kuzembea katika malezi ya watoto wao. Aliwasisitizia kuhakikisha wanawapa watoto wao malezi bora la sivyo watashughulikiwa na walinda usalama. "Wazazi tumefeli kimalezi ya watoto wetu. Utaachaje watoto wadogo kuzurura badala ya kuhakikisha wako shuleni kusoma? Lazima tuwajibike la sivyo tunapowakamata watoto wenu kwa uhalifu pia nyinyi tutawakujia," akasema Bi Onyancha. Hata hivyo alipongeza juhudi za walinda usalama kote Pwani akizitaja kusaidia pakubwa kumaliza au kupunguza uhalifu wa vijana wa mapanga kwenye kaunti kama vile Mombasa na Kilifi. "Tulikuwa na tatizo la utovu wa usalama uliochangiwa na magaidi wa Al-Shabaab. Hilo tulimaliza. Iweje leo tunaanza kuzuka na magenge ya mapanga na visu kuhangaisha umma? Hatutakubali kurudishwa nyuma. Wananchi tushirikiane kumaliza uhalifu," akasema Bi Onyancha. Gavana wa Lamu, Issa Timamy, aliyekuwepo kwenye kikao hicho alisema, “Tulimaliza mihadarati, hiyo shida ya magenge ya visu, mapanga na visasi pia tutaimaliza katika jamii," akasema Bw Timamy.
Go to News Site